#ALIPO ROHO WA MUNGU UPAKO UNAMIMINIKA KWA MAJIRA YA MUNGU NA WAKATI WAKE

Joshua na Karebu walikuwa watu wema walioripoti ukweli ambao ndio hali ilivyokuwa kule walikokuwa wanapeleleza na wakapata kibali kwa Mungu, hata mashushu wengine walivyopigwa kwa tauni kwa ripoti zao za uwongo wao walipona. Hesabu 14:38 katika biblia inasema “Lakini Joshua mwana wa nuni na Karebu mwana wa Jefune walibaki wazima pekee yao kati ya wale waliotumwa kwenda kupeleleza nchi ya kanani (ahadi).
Wakati Musa akifikiria ni yupi atakayeendeleza kazi iliyompasa yeye, biblia inasema katika hesabu 27:18-20; BWANA akamwambia Musa “Mchukue Yoshua mwana wa nuni, mtu ambaye roho yuko ndani yake, uweke mikono juu yake…….

Baada ya Musa kumuapisha katika Kumbukumbu la Torati 34:9; Joshua alijawa na nguvu na roho wa hekima na wana wa Israeli wakamsilikiza na akafanya vile Mungu alivyomuamuru Musa.
Ninajiuliza kwa nini isiwe Karebu, mtu mwema lakini neno linasema ndani ya Joshua kulikuwa na roho ile tangu kitambo. Hii inaonekana pia pale Musa alipowaita wazee 70 wa Israeli katika Hesabu 11:24-25; inasema sehemu ya roho ndani ya Musa ilipowaingia wale wazee nao wakaanza kutabiri, lakini hawakufanya tena.
Ndiyo maana nasema ambapo roho wa Mungu yupo upako au nguvu ya Mungu inamiminika katika majira ya Mungu na sio ya mwanadamu. Hata Yesu alikuwa na roho yule kwa miaka 30 lakini kabla alikuwa akiishi maisha ya kawaida mpaka pale Yohana mbatizaji alipotimiza wajibu wake kama ilivyoandikwa katika Mathayo 3:15-16 kutimiliza haki yote; Neno linasema Mbingu zikafunguka na sauti ya Mungu ikasikika kuthibitisha kwamba Yesu wa Nazareti ndiye mwanae mpendwa na baada ya hapo Yesu wa Nazareti aliongozwa na roho mtakatifu mpaka jangwani kwa maandalizi ya huduma yake aliyoifanya kwa miaka 3 duniani.
Kama laana inaweza kupatilizwa katika mtiririko ule ule wa damu kutoka kizazi mpaka kizazi ni zaidi kwa Roho mtakatifu mtoaji wa vyote, nguvu yake inaweza kutiririka kwa mwendo wa ajabu kama upako kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kwa majira yake Mungu.
Mwanzo 1:2 inasema……..na Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji. Kinachonishangaza mimi ni kwamba Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji kabla ya kupewa neno la kutekeleza kwa muda gani? Hakuna ajuaye ila Mungu mwenyewe, Ona biblia inasema siku moja ya Mungu ni kama miaka 1000 kwetu sisi tulio duniani(2 Petro 3:8), na kwa Mungu hakuna kitu kinachochelewa vitu katika ulimwengu waroho viko katika mwendo kasi wa ajabu katika utekelezaji wake.
Kwa fikra hii unakuwa ni yule roho aitendaye kazi ndani yako kiuhalisia wa macho ya nyama na si katika ulimwengu wa roho baada ya kumtambua yule roho ndani yako na katika majira ya Mungu alivyokusudia, nikimaanisha baada ya roho wa Mungu kujithibitisha ndani yako nawe kuwa na uhakika juu ya uweza uletwao na roho mtakatifu, ile mwili na nafsi na roho mtakatifu kuwa na umoja na sehemu ya maisha yako, roho mtakatifu anakuwa halisi katika maisha yako anakuwa ni kama wewe tu unavyotenda ndivyo roho wa Mungu akusudiavyo. Na roho wa Mungu ndiye mkuu na ndiye anayewezesha muunganiko huo kuwa dhabiti.
Na kama Mungu akisema hakuna awezaye kukataa hata mwili na nafsi yako mwenyewe haviwezi kukataa ama kuzuia kusudi la Mungu maishani mwako bali kulifuata ili likamilike kumbuka kwa habari ya Nabii Yona.
Unaona ilianza kwa Elisha kuwa Elisha lakini kwa sababu ya roho yule mtakatifu baada ya miaka 17 ya kumuelewa roho huyo kupitia Eliya, Elisha akawa Eliya na zaidi.
Na pia Yohana alianza kama Yohana lakini kwa sababu ya ile roho mtakatifu kwa miaka yote aliyokuwa nyikani akijifunza kumuelewa na kutunza maagizo ya roho yule aliyempokea tangu akiwa tumboni mwa mamaye, akaja kuwa Eliya ndio anaishi ndani yake.
Na pia Yesu wa Nazareti alianza kama Yesu wa Nazareti, neno pia linasema katika Luka 1:35; Roho Mtakatifu akamjilia Maria nazo nguvu zake yeye aliye juu zikamfunika kama kivuli roho akafanyika mwili ndani ya tumbo lake akawa mimba na baadaye Yesu akazaliwa kama wanadamu wengine. Hivyo ilimchukuwa miaka 30 yeye kukamilika na kuwa tayari kwa huduma aliyoijia duniani na lilipotimizwa tendo lililofanyika Mto Yordani Yesu wa Nazareti akathihirika kuwa ndiye KRISTO.
Ndugu uliyeokoka roho wa Mungu yu ndani yako na atatimiliza kile kilichokusudiwa maishani mwako duniani hapahapa. Hivyo rafiki usikate tamaa katika yale uyakusudiayo hakika kuna wakati wa Bwana ambao hakuna ajuaye ila roho wake.

Elimu ya Mungu ni ya ajabu sana, na roho wake ni mwalimu mwema na wakushangaza sana, visivyojulikana kujulikana kwetu na visivyoonekana kwetu kuonekana hii inashangaza sana, ndio maana Yesu wa Nazareti alisema ni maajabu ni miujiza ni ishara vitu ambavyo Mungu anatufunulia katika roho wake. Sema Mungu nipe ufahamu niweze kukufahamu wewe kwa kina na kuzijua njia zako kwa kiwango kile ulichonikusudia ili iwepo hekima ndani yangu na maarifa pia kupitia neno lako takatifu na kwa hivyo niweze kuibadilisha dunia ninayoishi.

No comments:

Post a Comment