#KUNEEMESHWA NA BWANA NI ZAWADI

    Siku zote kama mbuzi akifungwa sehemu moja kwa muda mrefu hata akiachiwa huendelea kukaa Sehemu zile zile na itamuchukua muda kuweza kuchukua hatua ya kwenda mbele zaidi. Biblia katika Waebrania 6:1-2 inasema; “Basi sasa tutoke katika yale mafundisho ya msingi kuhusu Kristo, tupige hatua kufikia ukamilifu katika kuelewa kwetu. Hatupaswi tena kuwaeleza ninyi yale mafundisho ya msingi kuhusu kutubu na kuacha matendo yaletayo kifo, na kuhusu kumwamini Mungu pamoja na maagizo kuhusu ubatizo, kuwekea watu mikono, kufufuka kwa wafu na hukumu ya milele.”

Ndugu mpendwa ukishajua hayo mafundisho ya msingi kuhusu kristo kuna hatua zaidi ya hapo kuiishi hiyo neema ipatikanayo katika Kristo, kuna matunda yanayoambatana na neema ya Mungu na kibali chake ukimcha Mungu na kumtii. Waraka wa 3 Yohana 1:2 inasema; “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.”

Hivyo Kuneemeshwa na Bwana ni zawadi kutoka kwa Mungu hakika, tunapaswa kuishi maisha ya mafanikio makubwa sana tuwapo na Kristo kinyume na hapo kuna kuwa na shida sehemu fulani. Ukisoma Mhubiri 5:11-12, 5:17 na 6:2 utaona jinsi ambavyo kuwa na mali nyingi bila Bwana kuwavyo na ubatili mwingi, mwanadamu kutofurahia alichotafuta, wageni kula jasho lake, taabu azipatazo pamoja na kuwa na mali nyingi halali usingizi, mawazo wengi, magonjwa na uchungu hakuna faida kubwa aipatayo.

Lakini Biblia hiyo hiyo inatujuza juu ya utajiri ulio na amani na mafanikio makubwa; ya kwamba si kingine bali ni zawadi ya Mungu, Ukisoma Mhubiri 5:18-20 inasema; “Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake. Tena, kwa habari za kila mwanadamu, ambaye Mungu amempa mali na ukwasi, akamwezesha kula katika hizo, na kuipokea sehemu yake, na kuifurahia amali yake; hiyo ndiyo karama ya Mungu. Kwa kuwa mtu hatazikumbuka mno siku za maisha yake; kwa sababu Mungu humtakabali katika furaha ya moyo wake.” Na pia Mhubiri 3:13 inasema; “Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.” 
Na ndio maana Mtume Paulo katika Waefeso 3:8 anasema "mimi niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa NEEMA hii ya kuwahubiri mataifa UTAJIRI WAKE KRISTO USIOPIMIKA", Kwa hiyo ni neema kuwa na utajiri usiopimika katika Kristo. Kwa maana hata Kumbukumbu 8:18 inasisitiza kuwa ni yeye tu Yesu atupaye nguvu za kupata utajiri.

Hivyo ni karama ya Mungu kuishi maisha ya mafanikio na baraka tele ndio maana hata Waefeso 4:8 inasema; "akateka mateka, akawapa wanadamu vipawa"; ndio hizo zawadi tulizopewa wanadamu alitujaza vyote fanikiwa ndugu katika Kristo Yesu maisha yako yasiwe ya kawaida, na ithihirike ulimwenguni kuwa Mungu wetu sio Mungu wa umaskini au uhaba au ukata bali ni Mungu wa utajiri, mwenye utajiri mwingi, na mali na kila aina ya ufahari. Tumwamini Mungu katika Kristo Yesu wa Nazareti ya kuwa anaweza na ndiye atutajirishaye kuanzia rohoni mpaka mwilini.

     Mungu na atujalie kuendelee mbele katika imani tuliyonayo katika Kristo [Waebrania 6:3], tuifikie maana halisi ya ukristo wetu ambao sharti udhihirike katika mwili wa Mwanadamu yale matendo, umiliki na utawala uliowekwa chini yetu na sio tu rohoni kama 3 Yohana 1:2 inavyosema. Bwana na akuneemeshe kila idara katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, Barikiwa!! kuwa MBARIKIWA na mwanajumuiya wa WABARIKIWA WA BWANA, Amina.

No comments:

Post a Comment