Sisi ni vyombo vya Yesu wa Nazareti, ni vyombo vya Bwana, Biblia inasema katika 2 timotheo 2:20-21; “Katika nyumba ya kifahari kuna vyombo vya dhahabu na fedha na pia vimo vyombo vya mbao na vya udongo. Baadhi ya vyombo ni vya heshima lakini vingine sio. Kama mtu akijitakasa na kujitenga na visivyo vya heshima atakuwa chombo cha kutumika kwa shughuli za kifahari; chombo kilichotakaswa kimfaacho Bwana wa nyumba, ambacho ni tayari kwa matumizi yote yaliyo mema”.
Usiache kuhudumia hali unahuduma ndani yako, Roho mtakatifu ndio huduma ya Yesu kristo wa Nazareti duniani kote, Yesu wa Nazareti alianza huduma ya kuwaunganisha wanadamu na Mungu kule Galilaya ambayo baada ya yeye kupaa mbinguni (ingawa yu hai ndani yetu), akaachilia Roho mtakatifu aiendeleze huduma ile ya Ufalme wa Mungu duniani ya kuwaunganisha wanadamu na Mungu, kwani alisema "Mimi ni njia, kweli na uzima mtu haji kwa MUNGU BABA isipokuwa kupitia kwangu".
Tangu Bwana alivyokuokoa wewe u chombo chake itende kazi yake kwa nguvu zako zote, kwa moyo wako wote na kwa akili yako yote huku ukijua ni Roho mtakatifu ndiye muwezeshaji pasipo yeye huwezi kufanya chochote utakachokukifanya kikafanikiwa (Zekaria 4:6).
Biblia tu ni muujiza ambao Mungu ameufanya, kule kuandikwa kwake vile maandiko yalivyotunza tangu enzi za Adam, wale watumishi (vyombo) vilivyotumika kuandika ni muujiza kwa kweli. Saa ingine nafikiria naishia kusema Mungu ni Mungu wa ajabu sana sana hakika njia zake hazichunguziki. Nalimsoma Ayubu biblia haizungumzii mwanzo wake kwa kina kwamba alitokea wapi?, uzao wake umeanzia wapi? na ni kipindi gani alikuwepo je ni enzi za Ibrahim au la! Lakini alikuwa mtu wa Mungu aliomba akasema (AYUBU 19:23-24);” Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa, Laiti yangeandikwa kitabuni, yakachorwa katika mwamba milele, kwa kalamu ya chuma na risasi.” Leo hii tunamsoma na maandiko yake hakika yana uvuvio wa roho wa Mungu, ona wakati mwingine unatenda kitu usijue lakini Mungu anajua kauli yako juu ya hicho ni muhuri wa moto wa Roho mtakatifu wewe ni chombo cha Bwana nena baraka na uhai. Biblia pia haizungumzii ya kwamba nani aliandika kitabu cha waebrania haijulikani, lakini kilikuwepo chombo cha Bwana kilichofanya kazi hiyo ambayo leo ni Baraka ya wengi, Mtu wa Mungu kinywa, ulimi, sauti yako ni vyombo vya Bwana hivyo maneno yako ni yana nguvu tamka leo ushindi kwa walioonea, waliovifungoni, wanaonyanyaswa, wenye shida, walio maskini, wenye kiu ya Roho Mtakatifu; Tamko lako ambalo ni NENO litaandikwa iwe kwenye karatasi, ufahamu, Mawe, daftari, Ardhini, CD, DVD au Gazeti lakini yeye Bwana Yesu wa Nazareti ataliandika kwenye mioyo yao kwa moto lisiondoke milele.
Nasoma Biblia, 1 wafalme 13:1-24; inamzungumzia mtu wa Mungu aliyetumwa kutoa onyo kwa Mfalme wa Israeli, baada ya kutekeleza agizo la Mungu kwa Mfalme, yeye mwenyewe hakufuata moja ya maelekezo aliyopewa kuyafanya akishatoka kwa Mfalme hatimaye akaliwa na Simba. Sisi kama Mtume Paulo asemavyo ni watumwa wa Mungu wasio na faida, ni punda wa Bwana, iwe unajua unachopaswa kufanya au hujui bado Mungu atakutumia kwa kazi yake, ili hata kwa wewe mtendaji ukishajua utukufu umrudie yeye Mungu. Nakumbuka kuna Sinema ya Yesu wa Nazareti imepata umaarufu sana afrika na dunia nzima na wengi wamebadili maisha na kumrudia Muumba kwa hiyo lakini Yesu wa kwenye sinema hiyo alikuwa anaigiza tu kama waigizaji wengine kama sehemu ya kujipatia kipato lakini wengi wameponya kwa kuigiza kwake kama Yesu wa Nazareti wameshika njia ya kweli na imani zao zimekua, lakini yeye hakuwa Mtumishi wa Mungu mwenye jina kubwa au mchungaji wa kanisa, ila anasema kuna siku waliopokuwa wanaigiza kukemea pepo mmoja alilipuka kweli na mapepo na haikuwa kwamba kweli wanafanya hivyo bali katika kuigiza tu. Kazi ya injili ya Yesu wa Nazareti ni kazi ya Bwana kupitia Roho wake mtakatifu, uwe unajua au hujui yeye Bwana aitenda kazi yake kwa majira na wakati wake, heri yule aliye na utayari nyakati na majira yote. Biblia inasema kuna nyakati zaja ambazo neno halitakuwepo kwa maana mafunuo ya rohoni hayatapatikana kinywani mwa wengi wawe watumishi wa Mungu au watu wenye hekima huku wengi wakiwa na kiu nayo hivyo yafaa sasa chochote kilicho cha uzima wa Mungu wafahamishe na wengine wapate kutoka gizani, hayo yapo kinywani mwako ili uyanene yaani ule ufahamu ule uelewe ambao Mungu ameachilia kwake kuhusu njia zake, kweli yake na uzima wake zipate kuishi mioyoni mwao. Kuna sinema nyingine imetoka mapema miaka ya karibuni ya mateso ya Yesu wa Nazareti (Passion of Christ) walioitengeneza ni watu wa kawaida sana na wana historia ya maisha ya tofauti hata si wachungaji au maaskofu lakini kupitia kazi njema ya mikono yao wengi wamevutwa kwa Bwana na bado wanavutwa kwake. Unakaa unafikiria ukiangalia dhambi zako, aliyoyatenda Yesu wa Nazareti kwa ajili yetu kwa picha za sinema hiyo moyoni unabubujikwa na kuomba toba, Hivyo itende kazi ya Bwana kwa majira yanayofaa na yasiyo faa huku ukijua ni yeye aitendaye wala si sisi, jina la Bwana libarikiwe, Amina.
No comments:
Post a Comment