#MWANADAMU AKIAMINI NI NGOME IMARA

     Hakika! Mwanadamu akimwamini Mungu ni zaidi ya ngome hata mwili wake huwa hauna uwezo tena wa kumumiliki ama kuyaendesha maisha yako, kwa namna ambayo thamani ya Uhai wake huwa ni Mungu mwenyewe na sio yeye mwenyewe. Ndio! Mwanadamu AKIAMINI waswahili husema ni shida, kwani hata mwili wake huwa mavumbi hakika hali yungai hai kwani huwa sio kitu tena kwake (huo mwili) cha kushikamana nacho hata atishiwapo kuuawa (Ufunuo 12:11), kwa sababu kumuamini Mungu ni nguvu za Mungu zisizoshindwa na kitu ama kuogopeshwa na kitu chochote ama mtu yeyote.

Nasema tena mwanadamu akiamini yaani akimwamini YESU KRISTO kuwa ni Mungu ndipo awezapo kiishi kwenye kiwango hicho cha uungu wa Mungu, kwa sababu wa nyama yaani mwanadamu hawezi kuwa mjasiri ama roho yake kuhuishwa mpaka aone mfano wa mwanadamu wa nyama kama yeye aliyeweza kushinda yote ndivyo naye ashindavyo, ndio maana kuanguka kwa Adamu wa kwanza kuliangusha wanadamu wote waliomfuata yeye yaani wale wote pamoja na sisi tuliofuata baada yake, lakini kushinda kwa Adamu wa pili yaani YESU KRISTO ndio kutuwezeshavyo sisi nasi kuwa washindi katika yeye. YESU KRISTO alikuja kama mtu wa nyama duniani hali yuna uungu ndani yake na ni Mungu hakika ili kutuonyesha na kutufundisha sisi mwanadamu tuliovunjika moyo na kukosa matumaini namna ya kuishinda dunia, ndio! dunia inapaswa tuishinde kwa kuwa ni adui wa Mungu (Yakobo 4:4), ndio! Giza lahatamia dunia na kuzaa mapooza lakini yeye alikuja kama Nuru ulimwenguni ili kila aliyejaliwa kwa neema ya Mungu kuiona hiyo Nuru asikae tena gizani bali apate uzima wa milele kwa kuiamini hiyo Nuru iliyofunuliwa katika Kristo YESU.
Unaweza ukashindwa kuelewa ya kuwa nazungumzia nini hapa, naomba kwa neema zake Mungu akufunulie kwa uwezo wa Roho mtakatifu katika jina la YESU KRISTO nawe upate kumwamini Mungu. Nasema tena na tena mwanadamu akiamini yaani “WHEN MAN BELIEVE” ngoja nikwambie hivi siyo MWANADAMU AKIAMINISHWA namaanisha AKIAMINI yeye kama yeye, yeye mwenyewe akimwamini MUNGU hapingiki msimamo wake, hakati tamaa, haogopi kitu wala mtu hata iwe malaika amshawishie mabaya, ndio! Mwanadamu akiamini.

Kuaminishwa ni kuzuri lakini ni moto wa muda tu kama utaishia kutokumuamini Mungu aliye wa milele yaani kama imani yako itagota kumuamini tu yule aliyekuaminisha kwa Mungu ambapo wewe mwenyewe pengine usimjue mungu huyo. Kuaminishwa ina maana sio wewe mwenyewe unapewa nguvu ya kuamini bali mtu mwingine anakuwa ana nguvu ya kukuaminisha wewe yaani unakuwa unamwamini Mungu kwa sababu fulani kasema kitu cha ushawishi cha kukufanya wewe uamini lakini moyoni mwako wewe kama wewe huna mizizi ya imani hiyo hii ni mbaya sana, kwani wale wakuaminishao kama tu watakengeuka kwa namna yoyote ama kupotoka wataanguka na imani za wengi na kuwafanya warudi nyuma kwa sababu hawakuamini kwanza katika Mungu bali waliamini kwanza katika mwanadamu kisha Mungu, imani yao ikawa inavutavuta huku ikiwa imeshikiliwa na wale walio waaminisha. Ndio! Kuaminishwa na wanadamu baadae kisha wewe mwenyewe kumuamini Mungu ni sawa na ndio mpango wa Mungu na haipingiki na inawezekana kabisa, ila sasa wapo walioaminishwa kwa mungu ambaye hawamjua wakamwamini yule mwanadamu kisha akawaingiza wote kama kondoo korongoni na wapo walioaminishwa wakaishia kuwa kama wapambe wa wanadamu hao ambao mwisho wao haukuwa katika mpango wa Mungu bali wa mwanadamu hawakuwa na msingi wa Neno la Mungu wala mizizi iliyoshikamana na Mungu bali kama upepo usio na uelekeo uelekeao pande zote.

Ndio maana YESU KRISTO anasema; Je’ kutakuwepo na imani duniani wakati Mwana wa adamu atakaporudi?(Luka 18:8), Jamani kuna imani nyingi duniani lakini ipo imani ya KRISTO ambayo ni hakika kabisa tunayopaswa kushikamana nayo milele, wengine waweza sema imani yako imepunguka ama imeisha kabisa lakini wewe rohoni unajua unayoimani inayoongezeka kila wakati ambayo wao hawajaifahamu bado, unajua kwa nini? Ni kwa sababu zipo imani nyingi duniani. Natujue kabisa hatuweza kumpendeza Mungu pasipo imani ile ya kumuamini yeye Muumba wa vyote (Waebrania 11:6), na pia YESU KRISTO anasema yeyote asiyeipoteza ile imani ya kumuamini yeye amebarikiwa hakika (Mathayo 11:6), kwa hivyo ili kweli tuwe na haki mbele za Mungu (wenye haki) imetupasa kuishi kwa imani yaani tuishi tukimuamini yeye na wala sio miungu (Wagalatia 3:11).


Mpendwa mwamini Mungu hata kama ni kupitia mwanadamu lakini nakusihi mwamini Mungu sana sana ili usiweze kutikiswa na nguvu batili zilizoenea ulimwenguni ama kuaminishwa katika imani itakayokuondolea haki ya Mungu, na Mungu atuwezeshe na kutuweka katika mikono salama ya wanadamu wake aliowaandaa na kuwakusudia yeye mwenyewe kuwa kama viongozi kwetu na sio wale wanadamu ambao kwa kuteka nguvu za dunia ama kwa upako wa Mungu waliouchafua usio na utukufu wa Mungu tena wakajifanya viongozi juu yetu ili kututawala. Bwana YESU KRISTO yu hai mwamini yeye leo atakuwa salama yako na ukombozi wako na uzima wako na uponyaji wako na mafanikio yako, Amina.

No comments:

Post a Comment