#MAISHA NDANI YA YESU

Ni kwa namna gani nalimjua Yesu ya kuwa yu mwema?, huu hakika ni upendeleo wa ajabu na mkuu sana na ni kweli ya kwamba Mungu ni pendo. Maisha ndani ya Yesu kweli ni kuwa kiumbe kipya na hakika ni kuzaliwa mara ya pili. Nimetendewa nimeona na nakushuhudia ya kwamba hakika Yesu kristo ni Bwana. Adam wa pili - Mungu kuvaa mwili na kukaa nasi, Na kwa neno lake dunia iliumbwa na vyote viijazavyo. Yeye aliye kuwepo kabla ya vyote, aliyenuru aliamuru Nuru iwe kutoka katika Giza nayo Nuru ikawa na kufanya usiku na mchana kutupendezesha na kutustarehesha sisi tulio viumbe vyake. Alifanya vyote viijazavyo dunia kutoka ambavyo mwanzo havikuwepo. Hata niwapo kimya pasipo kusema neno, roho yangu siku zote yashuhudia matendo makuu ya Mungu na ya kwamba Bwana Yesu Kristo ametenda miujiza ndani yangu na kubadilisha maisha yangu kabisa.
Sikuwa mwema sikuwa safi sikuwa mtakatifu nalichafuliwa na kujichafua tangu mwanzo nilipofungua macho yangu kutazama katika hii dunia. Lakini Yesu kristo mwingi wa rehema, alinihurumia na kunisafisha kabisa kwa damu yake ya thamani iliyomwagika pale msalabani, Biblia yasema ni kwa neema tu tunapokea uzima wa milele sikupanga, sikujua lakini yeye alijua na hata iweje nisingepanga,  kwa kweli Bwana Yesu ni mwema sana. Kwa maana kwa kupiga kwake nilipona hakika na kifo chake cha msalaba kilihitimisha yote; yaani yote yalikwisha pale Golgotha.
Ufunuo 12:11 yasema; “Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao, kwa maana hawakuyapenda maisha yao mpaka kufa”.  Naukumbuka wokovu wa maisha yangu mwezi wa pili, 2008 nami nalijua nakumfahamu Mungu ya kwamba ni mwema na ananijua kwa jina. …. mwanadamu kuzaliwa mara ya pili kwa roho mtakatifu huwezi kuelezea vizuri jinsi inavyokuwa kama Yesu alivyosema ni kama upepo uvumao mashariki kwenda magharibi huwezi sema huu hapa au ule pale lakini utaona matokeo yake matawi ya miti kupukutika, vitu kupeperushwa na huo ndio ufalme wa Mungu ujavyo ndani ya mwanadamu-Vitu vya kimwili vilivyozoeleka tangu utoto kusimama hapo na vitu vya kiroho kuanza hapo.
Inashangaza na ni kweli kwamba kumutumikia Mungu kuna faida sana. Biblia imeandika Yesu aliwatuma mitume wake waende mji wa jirani nao watamkuta mwana punda amefungwa, wakiulizwa kwa nini mnamufungua akawaambia semeni ”Bwana ana Haja nae” nami naamini hakika nalikuwa nimefungwa na vifungo vya dunia hii vya magonjwa, utumwa wa kila namna, kifikra, kimtizamo, kimawazo, kiroho, kinafsi, kimwili. Lakini Bwana Yesu kristo kipitia mitume wake aliniweka huru kwa kuwa hakika anahaja nami hata sasa. Siku zote utayari unamengi yafaidishayo ona mwanapunda yule, Yesu kristo alimutumia katika huduma alipokuwa anaingia yerusalemu na ule utukufu alioingia nao kule yerusalemu hata punda naye alitembea katika huo walipomtukuza yeye na kumheshimu kwa kushangilia, kuweka matawi, kutandika nguo ili Yesu apite juu yake hata punda naye aliipata heshima ile kwa wakati wote aliokuwa na Yesu wa Nazareti, kwa hiyo faida ipo kutumika ndani ya kristo ndio neno lasema ni mizuri kama nini miguu yao wao wahubirio ufalme wa Mungu ile injili ya Yesu Kristo.
Tatizo ni kwamba ujio wake ni nani atambuaye? Yesu alipouangalia mji ule wa yerusalemu akalia na kuhuzunika sana na kusema ee! Yerusalemu kama tu ungejua kujiliwa kwako/ ile siku ikupayo amani ungekuwa tayari kuupokea ufalme wa Mungu, lakini yote yamefichwa machoni pako tazama utavunjiwa ukuta wewe na familia yako wala halitabakia jiwe juu ya jiwe. Ndugu nakutia moyo siku zote kuwa tayari kumupokea yeye aliyetupa pumzi ya uhai kwani neema yake ni kuu kwa yeye aaminiye aliyemnyenyekevu na mtiifu katika kutenda yaliyo ya haki na mema.
Najifunza sana kwa habari ya Musa katika biblia, ndugu zake walihofu kuwa angeuawa na Farao wakamficha kwenye kisafina. Mungu ni mkuu sana ndugu wazazi wawezadhani wanaulinzi juu ya maisha yako lakini zaidi ni maagano na mizigo tu wanayoweza kukuwekea kwani neno lasema amelaaniwa mtu yule amutegemeaye mwanadamu kumfanya kuwa ni kinga yake.  Msisitizo wa Biblia ni huu kwamba utaijua “kweli” nayo kweli itakuweka huru, yaani ile kweli utakayoijua ndio kwa hiyo utakuwa huru na sio kila kweli kwani biblia yote ni kweli, Sali sana uijue kweli ya Mungu uwe huru kwa maana neema yake yatosha. Na kama Waraka wa kwanza wa Yohana 2:27 inavyosema kuwa; “nanyi, mafuta yale (upako) mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake (upako) yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake”.
Kwa hivyo ndugu pokea hayo mafuta/upako kwake leo, mwamini Yesu wa Nazareti akuweke huru na umjue vizuri Mungu wako na kufahamu njia zake, kwani yeye ni Mungu wa kuokoa; na njia za kutoka mautini zina yeye Bwana (Zaburi 68:20), yaani ni yeye pekee awezaye kukusamehe dhambi na kukupa uzima wa milele kwa kuwa yeye ni Mungu na Baba wa milele.
Jina la Bwana libarikiwe!
Shout JESUS!!, The Mighty Saviour, Amen.

No comments:

Post a Comment