Muda mrefu nimekuwa katika fikra na hili
limekuwa jambo gumu na kubwa ndani yangu huku imani katika kristo ikiwa ndio
chachu kuu katika hili. Nami nikawa
najiuliza kwa muda sasa ya kuwa imani halisi ni ipi ipaswayo kufuatwa, kwa
sababu wengi sasa wanakata tamaa zaidi hata kabla ya vile walivyokuwa
wanajihusisha na makanisa ya kiroho, na wengine vijana kwa wazee wamethubutu
hata kurudi nyuma na kufuata makanisa ya
awali waliyoanza kusali kabla ya kuwa na utashi huru yaani kule mababa zao na
mama zao walikokuwa wanasali, hii ni hali halisi kabisa kwa kanisa la Mungu la
Tanzania. Nami moyoni hili hunisononesha sana, na hujiuliza hivi je imani ya
mwanadamu yaweza kukuzwa ama kuuawa
sababu ya kanisa mtu asalipo? Na’ je kushuka ama kupanda kiroho/kiimani huwa ni
kwa sababu ya kanisa, ama mtu mwenyewe ama mchungaji na viongozi wengine wa
kanisa?
Na je Imani ni nini
hasa?, Biblia
inasema Imani ni hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana
(Waebrania 11:1). Hivyo imani ni kule kufumbua fumbo, mwanzoni kuna uwezekano mkubwa
mtu kuamini kwa namna ambayo inakinzana na maana halisi ya Mungu mwenyewe jinsi
alivyotaka. Ndio maana utaona katika warumi
8:14 biblia inasema wanaoongozwa na roho
mtakatifu hao ndio wana wa Mungu, kuna changamoto hapo, maana yake ni
kwamba pasipo yeye unaweza toka nuruni na kwenda gizani hali ungali na shauku (Luka
11:35-36) hata pasipo kujua saa ingine (1 Wakorintho 10:12). Na katika
waebrania 10:38 ameweka hadharani kabisa “lakini
mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisitasita roho yangu haina furaha
naye”.
Ndio maana somo hili ni bufe la imani
ikimaanisha imani ni nyingi duniani na nafsi ya mtu huchagua kwa kuamini; na ni
kivipi kuamini; kwa maana mtu ni nafsi huru kama biblia inenavyo na Ukristo
halisi ni kwa neema ya wokovu ipatikanayo kwa kumuamini Yesu kristo. Yesu
katika biblia anafafanua kuhusu suala la imani, katika Luka 18:7-8 Yesu
anasema; “Na
Mungu je’ hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Naye ni mvumilivu. Nawaambia, atawapatia haki
upesi, walakini atakapokuja mwana wa
Adamu, je ataiona imani duniani?. Ona hapo anasema kwa habari yake mwenyewe
kama nabii ya kwamba je
atakapokuja duniani ataikuta imani. Imani ipi sasa? Anamaanisha ILE IMANI
ambayo yeye aliiacha duniani, usemi wake huo unaonyesha shaka aliyonayo juu ya
wanadamu na misimamo yao juu ya Imani halisi katika yeye. Na ndio maana Ufunuo
3:11 inaanza kwa kusisitiza ‘naja upesi’ shika sana ulichonacho asije mtu
akaitwaa taji yako, hivyo imani hupokelewa na mtu na hupaswa kutunzwa na
kuitetea isife ndani ya mtu huyo. Biblia katika Yohana 17:3 anasistiza kuwa; “uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe
(MUNGU wa pekee wa kweli) na Yesu Kristo uliyemtuma”. Hiko ndio chanzo cha
imani yetu kama wakristo yaani kumuamini Mungu na Yesu Kristo aliyetumwa kwetu.
1 wakorintho 13:9 inasema“kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu”, ingawa sasa katika uhalisia mwanadamu kwa
hiyo sehemu anayoifahamu hudhani anajua yote. Cha msingi mtu kujua ni kwamba dini ya
kweli ni ile kweli ya Mungu, ambayo mtu huiamini au hupaswa kuiamini.
Mungu wa kweli; hata mashetani wanamfahamu, wanamwamini
na hata wakimuona au kusikia jina lake wanatetemeka (Yakobo 2:19), hivyo
udhihirisho wa imani yako kule kumwamini Mungu hudhihirishwa na matendo yako,
sasa kutotenda sawa sawa ni dhahiri kwamba imani ndani ya mtu huwa imehadaiwa.
Kwa maana imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la kristo
(warumi 10:17), kwa hivyo imani chanzo chake lazima mtu asikia neno la Mungu,
vinginevyo ni upotofu.
Imani nyingi zinazoelezwa kuenea ni kutokana na
wapinga kristo wengi ambao wamekwisha kuwapo duniani (1 Yohana 2:18). Tatizo
sasa kuhusu ukristo halisi na hili suala la bufe la imani sio juu ya wachungaji
ama kanisa bali mtu mwenyewe, maadamu biblia imeeleza uwepo wao. Suala ni mtu
mwenyewe; anatakiwa asikie neno la kristo ndipo aamini na sio maneno mengine na
kumuamini Mungu pekee yake na Yesu kristo aliyetumwa kwetu na sio kingine. Na
ijulikane kabisa wokovu ni kwa neema na ni Baba wa mbinguni ndiye humuokoa mtu
na wala si mwanadamu. Hatuendi tu kwa Mungu bali yeye hutuvuta kwake kwa neema
yake, ila sharti tuamini kwamba Mungu yuko (waebrania 11:6).
Na tamaa zako sio kipimo kwamba unampenda Mungu,
(1 Yohana 2:16-17) hata kama utakuwa unaenda kanisani, hivyo shauku yako
huangaliwa kama kweli unamwamini Mungu wa kweli, nia ya mtu kwa Mungu ndio
hupelekea mshikamano na Mungu, kama sivyo basi ni tamaa na tamaa ya vya dunia
huvita vya dunia (Warumi 1:24) ikiwa pamoja na imani za wapinga kristo. Uhakika
ni huu ya kwamba ukimwamini Mungu wa kweli huwezi potea njia kwa maana nia yako
na mawazo yako yatakuwa wazi mbele zake na matendo yako kuthibitika naye
hatakuacha upotee milele. Na biblia katika 1 Yohana 2:17 inathihirisha ya kuwa mwanadamu
atadumu hadi milele kwa kuyafanya mapenzi ya Mungu.
Biblia katika Efeso 1:3 -7 inatuhakikishia kuwa
wokovu uliojua ndani yako ni halisi kabisa, na ndiye kristo kwa neema yake
alikujalia kuwa nao na ndiye aliyetuchagua kabla ya kuwekwa misingi ya
ulimwengu. Kwa hivyo wokovu ni wa mtu binafsi ila sasa unaokolewa na Bwana ili
uokoe wengine kuanzia na familia yako yaani watu wa nyumbani mwako, umeokolewa
ili kutangua misingi ya vizazi vya kale iliyo kinyume na kusudi la Mungu
duniani na kuvunja madhabahu za miungu ya ukoo na kujenga misingi mipya na
madhabahu mpya inayomtii na kumuamini Yesu Kristo ya kuwa ni Mungu pekee
asitahiliye kuabudiwa na kila kiumbe. Kama Gedioni katika waamuzi 6 pale
alipookolea tu na Bwana akatangua madhabahu ya baba yake na mababu yaani zile madhabahu
ya miungu kwa maelekezo ya malaika wa Bwana akatoa dhabihu kutangua dhabihu za
damu za watu na wanyama zilizomwaga katika madhabahu zile, na kisha akafanya
madhabahu mpya kwa dhabihu safi ili Yesu kristo atukuzwe kwenye ule ukoo na
jamii kwa ujumla na ikawa hivyo.
Yesu kristo alikuja na agano jipya ndio! Lakini
kuwapo jipya hakukufutilia mbali lile la kale alilifuatilia kwa kina na
kutangua panapostahili na kukazia palipopaswa kuondoa mapungufu yote ili kuwepo
ukamilisho katika lile lililo jipya. Niseme nini sasa, wokovu ni uhuru wa nafsi
ya mtu katika dunia ile ile iliyo na uovu ambao bado unakuwa unafuatilia nafsi
ile ile iliyowekwa huru na Bwana, Ndio! Nimeokoka ila ukoo wangu bado, hapo jua
kuna kazi ya kufanya ili uhuru wako uwe kweli na hakika, wokovu wako hauna taji
kama hauthihirishwa au kupimwa kwa kazi uliopaswa kuifanya.
Imani ni nyingi duniani, na kuna ukristo halisi
na imani halisi kabisa ambayo Bwana Yesu Kristo aliikusudia, na ndio maana hata
mwanzo wa huduma alionyesha mzigo aliokuwa nao juu ya imani zilizokuwa ni kama
zinawafunga zaidi kondoo badala ya kuwafungua na kuwafanya huru, na ndio maana
hata tamko la Isaya 61:1 alilisema kanisani na sio njiani wala sokoni bali
hekaluni mwa Mungu kondoo wanakokusanyika na kusikia Neno la Mungu. Na ye Yesu
wa Nazareti alisema Roho ya Bwana MUNGU i
juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari
njema; amenituma ili kuwaganga
waliovunjika moyo, kuwatangazia
mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Hili
tamko ni kubwa sana ina maana waliofungwa walikuwepo kanisani, waliovunjika
mioyo walikuwepo kanisani na mateka walikuwepo pia. Na sasa wapo kondoo
waliokuja na vifungo hivyo lakini pia wapo ambao vifungo vilizidishwa hapohapo
kanisani walikojua ni msaada kwao, kutokana na jinsi walivyojengewa imani na
viongozi wachungaji wa kanisa ama kutokana na Neno la Mungu jinsi vile
walivyokuwa wanafumbuliwa, kuaminishwa ama kutafsiriwa..... Si la kushangaza
sana hata Yesu wa Nazareti pale alivyowaita mafarisayo, masadukayo, waandishi,
waalimu wa sheria kuwa ni wanafiki! Kwa kuwa wanafanana na makaburi yaliyopakwa
chokaa, nayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya
wafu, na uchafu wote (Mathayo 23:27).
Ndugu mpendwa katika Bwana; Ukristo halisi na
imani isiyo na ukengeufu ni kuongozwa na ROHO MTAKATIFU huko ndiko kutakufanya
wewe uwe MWANA WA MUNGU (warumi 8:14) na uishi kama MFALME katika hii dunia,
Barikiwa na Bwana Yesu Kristo, Amina.
No comments:
Post a Comment