Duniani
kuna makwazo, shida na dhiki sana lakini kama biblia isemavyo jipe moyo kwa
kuwa Yesu aliushinda ulimwengu na ni hakika yetu nasi kushinda tukiwa ndani
yake Yesu, kwa maana makwazo yapo lakini imetupasa tuyashinde kwa mema na neno linatoa
ole! kama onyo kwa yule ayasababishayo.
Yusufu
nduguze walimkwaza sana yaani kila alipotaka kuzungumza jambo ambalo ni la
Mungu kwa faida ya familia yake nduguze walimpinga na kumchukia sana,
wakamtenga na kumfanyia mengi yakwazayo, yusufu alisonga mbele akimwamini
Mungu ilifika wakati wakampiga vita kiasi cha kutaka kuutoa uhai wake kisa tu
anayo neema na kibali cha Mungu lakini mwisho wa hayo yote ushindi ukawa dhahiri kwake.
Pia
tunamsoma Ayubu vile alivyovunjwa moyo na kukwazwa sana na mke wake na rafiki
zake kiasi ambacho yale majaribu yake isingekuwa neema kuu ya Mungu juu yake
yamkini asingeweza kupita kutokana na makwazo hayo, mke aliongea yake na
marafiki pia nao waliongea yao lakini yeye imani yake kwa Mungu ilikuwa kuu
sana kiasi ambacho kwa kule kuwa na kila kitu halafu ghafula kukosa vyote
hakukumfanya yeye amukufuru Mungu. Aliisimamia imani yake kwa Mungu katika
shida na raha pamoja na makwazo yote hakuteteleka akajipa moyo mkuu na
kujifariji mpaka akayashinda na wala hakuuchukua ushauri wa yeyote alikuwa yeye
na imani yake kwa Mungu ndivyo vilivyompa moyo wa subira na kumfanya adumu
katika ile imani na Mungu mwishowe akambariki maradufu.
Yesu
Kristo ambapo Mungu alijifanyisha mfano wa mwanadamu na kuishi pamoja nasi kwa
njia ya Yesu Kristo, aliishi maisha ya kawaida ya kibinadamu katika viwango
vyote tuvipitiavyo na akaonyesha unyenyekevu na utii mkubwa sana kwa Mungu vile
itupasavyo nasi kuishi mfano wake yaani yale maisha yake. Ndugu zake pale
alipokuwa anatimiza kusudi lake la kuishi duniani walikuwa wakimkwaza pia na
kutaka kutomuelewa kabisa ayapasayo kutenda duniani kiasi ambacho uhalisia wake
wote hakuuonyesha nyumbani kwake bali ugenini na kwa watu wa kuja waliomwamini.
Yesu
Kristo anajua katika makwazo, katika kuvunja mtu moyo ama kumupuuza kuna
kufifisha na kuua kusudi la Mungu katika maisha ya viumbe vyake ndio maana
aliasa katika Biblia kwamba waacheni watoto wadogo wamuendee yeye Yesu yaani
wale waliomwamini na kuwa na kiu ya kutenda mapenzi ya Mungu na akasema mtu
awakwazaye walio wadogo kama hao ni bora angefungiwa jiwe la kusagia na kutupwa
baharini kuliko kuharibu na kudhoofisha kwa namna yeyote ile; dhamiri zao
kuhusu Yesu kristo na utakatifu na imani yao kwake.
Ingawa
kwa wanadamu ndio kawaida yao tena hasa wale wanadamu wa karibu yako
watakuchunguza na kuangalia mwenendo wako na kisha kukujaribu wakiona kuna kitu
wataanza kukuvunja moyo na kukupuuza, halafu wataanza kukucheka kwa
maneno ya hapa na pale kisha wataanza kukupiga vita kila upande mwishowe
unashinda. Hivyo ndugu usikate tamaa
wala kuvunjika moyo kwa maana katika kuvunjika moyo kuna kudumaa kiroho na
kunajenga roho ya kujinyanyapa na pia kunaondoa ujasiri wako kiimani. Jua kuwa makwazo ukiyaruhusu ndani yako kunaongezeko la mawazo ambayo huondoa chocheo la imani rohoni na
kukujengea moyo wa kughairi na kukata tamaa saa ingine. Na makwazo hakika ni silaha ya shetani hata
kama itatumiwa na mtu ambaye ni kiongozi wako au yule anayesimama mbele zako, kwa kuwa yanaweza kufifisha ama hata kuua majaliwa yako
uliyopangiwa na Mungu kama tu utaruhusu makwazo yakutikise katika msimamo wa
imani yako.
Yote
katika yote yatupasa tumtazame Mungu mwenye enzi yote ndio kila kitu, kwa maana yule mkuu mbele
yako aliyefanyika nafasi ya juu, umuchukuliaye kama bwana wako anaweza kuwa
chanzo cha kukuinua ama kukuua kiroho na kisha kudumaza imani yako na mwisho kusudi la Mungu
lililokuwa angavu mbele yako kufifia ama kutoweka kabisa lisiwe majaliwa yako.
Biblia
inatufunza ya kwamba wale wajibidiishayo katika kuwaelekeza wengi katika njia
ya haki yaani namna ya kuishi maisha matakatifu hao watang’aa kama nyota. Hivyo
ni bora kuwa muhuishaji kuliko kuwa mfifishaji yaani kufufua na kuvifanya
viishi vya rohoni vilivyokufa katika wengi pasipo fikra potofu kuliko
kuvififisha na kisha kuviua kabisa vya rohoni vinavyotaka kuishi katika Bwana.
Kwa hiyo basi kuna nguvu na dhawabu kubwa katika kuinua wengine kuliko kuwafifisha
na kuwaua kiroho maana damu yao itatakwa mikononi mwao wafanyao hivyo.
Mungu
baba katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti tupe moyo huo wa kuinua wengine na
kushinda makwazo yote kwa mema kama biblia isemavyo tuushinde ubaya kwa wema, kuilinda imani yetu na kuwa wa upendo na
baraka katika wewe, Ameni.
Rejea katika Biblia;
Mwanzo sura ya 37-50 (kwa habari ya Yusufu), Kitabu cha Ayubu, Yohana 16:33, Marko
10:13-15, Luka 17:1-2, Danieli 12:3 na Rumi 12:21.
No comments:
Post a Comment