#JAWABU LA MAMBO YOTE, PESA!?

Hebu tazama mabarabarani, mashambani, majini, misituni, milimani, miambani, makorongoni, mashimoni, angani, mipakani, chini ya ardhi, mapangoni, kwa waganga japo nao wanayao mahangaiko ya pesa, vijijini, mijini, jumuiyani, makusanyikoni, mashuleni, vyuoni, vilabuni, kwenye kamari, bahati nasibu na kubeti, magengeni, masokoni, madukani, makazini, maofisini, mitandaoni, siasani, utafitini, serikalini, nje ya dunia, mchana na usiku utaona mahangaiko mengi ya wanadamu siku zote za maisha yao yametawaliwa na utafutaji wa pesa. Na hilo limekuwa jaribu kubwa mno kwetu ukizingatia nafasi ya Mungu Muumbaji wetu ya kumuabudu, kumsifu na kumtukuza maishani mwetu imewekwa wapi katika hayo na kwa asilimia ngapi ya muda wetu wote?. Hapo utaona fumbo lililo kwa mwanadamu duniani ni gumu mno juu ya pesa na mahangaiko yake, ushindani na kule kutoridhika nazo, je ni sisi wanadamu tumejifikishi hapa, ama tumetegwa tukwame katika hilo, ama ni matokeo ya nyakati na zama zake, na kama ni zama ni nani mchochezi wa hizo? Naje lapindishwaje sasa kusudi la Muumba, ni hivi ndivyo tulipaswa tuwe na tuishi duniani kwa sababu hii ya kutafuta pesa na matokeo yake?.
Waweza endelea nawe kutafakari katika hayo ili yamkini uione vyema nafasi ya Mungu maishani mwako i wapi?, lakini sasa ukisoma biblia inatujuza kwa habari ya pesa Mhubiri 10:19 yasema pesa ni jawabu la mambo yote. Mfalme Sulemani alipata ono la Neno hilo la Bwana akaiishi hiyo baraka katika imani hiyo, hata hivyo mwisho alikuja kujua kuwa pesa na mali nyingi sio vyote katika vyote (Mhubiri 5:11-12, 5:16-17 na 6:2). Na ndio maana Mhubiri 5:10 inasema apendaye fedha hatashiba fedha kwa maana ni karama ya Mungu kule kuridhika na ni fungu lake kwako. Hivyo pesa inatupa tu jawabu juu ya jambo, kwa maana nyingine palipo pesa pana utatuzi wa kitu au jambo na kutoa jawabu. Lakini mwisho wa yote Mathayo 6:33 inatuasa ya kwamba tutafute kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote tutazidishiwa, pesa kama pesa haiwezi kukupa ufalme wa Mungu (i.e. Mungu na ufalme wake) wala uzima wa milele na ukiwa mtumwa sana wa pesa inaweza kukupelekea pabaya na hata kuharibu imani yako katika Mungu muumba wa mbingu na nchi na vyote viijazavyo, ndio maana Mt. Paulo kwa waraka wa Timotheo ameonya kuwa kupenda sana pesa ni chanzo cha uovu (1 Timotheo 6:10). Na hii ni kawaida kwamba chochote kikizidi sana ni hatari ndio maana tunaaswa tuwe na kiasi katika kila kitu, hata Mfalme Sulemani katika Mithali 30:7-9 alisema BWANA usinipe umaskini wala utajiri bali alihitaji kiasi cha saizi yake ili asije kumkana au kumkufuru BWANA.

Sasa Biblia inaposema Pesa ni jawabu ina maana pia ni kama means itakayokuwezesha wewe kutambua jambo, ama ni kama kigezo au kitestio cha kukuwezesha kufumbua kitu ama pia kukupa namna. Sasa kwa nini pesa ni kama means ama kitestio tafakari pamoja nami kwa mifumo hiyo hapo chini ambapo ni muhimu kujua hivyo ili uweze kuwa na ufahamu hodari, sababu ni kweli pesa kama jawabu;
1) Huweza kutumika katika kufumbua uhalisia wa mtu (it can reveal true character of a person).
2) Hudhilisha namna mtu alivyo pindi tu awapo nazo kama ni mtoaji itajulikana.
3) Huonyesha namna mtu alivyomnyenyekevu na mtiifu (Humble and Obedient). Ndio maana uzoefu unaonesha mwana wa mfalme awapo mtiifu na mnyenyekevu haina shaka kabisa ndivyo alivyo bali maskini awavyo hivyo kuna walakini mkubwa.
4) Huonyesha na kudhihilisha kama nafsi yako imeshikiliwa na spiritual entities zozote ambazo hazitokani na Mungu. Kwa maana ujio wa pesa kwa mtu kwa kiwango cha juu ambacho hajawahi kukishika huprovoke reaction itakayofumbua yaliyo nafsi mwa mtu huyo, nikimaanisha kuwa pesa ni kama kitestio ama catalyst i.e. kichochezi cha kufunua jambo, hivyo ukitumia pesa utapata jawabu na matokeo.

Pesa ni tokeo au matokeo ya kile ulichokifanya. Na hivyo kufanikiwa sio kupewa pesa ama zile pesa zenyewe, bali ni kule kufunguka kwa ufahamu juu ya jambo litakalokupelekea kwenye upataji wa hizo pesa tena na tena, ule mfumo unaoutendea kazi hadi kuzivutia pesa kwako. Mfalme Sulemani hakuomba Mungu kupewa pesa na mali nyingi (matokeo) bali aliomba hekima (chanzo) ambayo itamuwezesha  kuvuta vyote  atakavyo ikiwemo pesa. Biblia inarekodi kuwa baada ya hayo maombi kwa Mungu Mfalme Sulemani alifanya madini kuwa kama mawe Israeli ilihali nchi hiyo haina asili wala historia ya kuwa na madini ardhini mwake. Kwa hivyo hekima aliyopata ilikuwa na upako wa kuvuta ama kufanya habari zake kutawanyika pande zote kwa sifa na kisha kumvutia utajiri wa kila namna.
Hivyo Mungu anaposema nitakubariki na kukufanikisha kiuhalisia hakupi pesa wala mali bali ufahamu na mafunuo yaani hekima yakukufanikisha na kisha kukupa mali ikiwemo na pesa (matokeo).

Lakini jua kuwa pesa na mali zikizidi sana usipokaa sawa zinaweza kukengeusha moyo wako na ukawa kinyume na Mungu. Mungu anajua hilo, ya kuwa moyo wa mwanadamu unatendency ya kuinukaga tu, hivyo unapaswa uwekewe technigues za kuufanya uwe unashuka. Hivyo kama ulinzi na usalama kwa wafalme wote wa Israeli Mungu aliwapa onyo hili katika Kumbukumbu 17:16-20 kwa habari ya kila mfalme wa Israeli akasema; "Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa BWANA amewaambia, Tangu sasa asirudie tena njia ile, wala asijizidishie Wake ili moyo wake usikengeuke wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno. Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika kitabu, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani walawi, na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi ili apate kujifunza kumcha BWANA Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya; moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kulia wala wa kushoto, ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe katikati ya Israeli."

Kwa hivyo basi katika yote kama kupenda penda zaidi kuwa na hekima maana Hekima ni Bwana (Mithali 8:12,14-32), naye ni ufunguo wa yote ikiwemo pesa, mali, biblia inasema ni mfano wa urithi, nayo ni bora kwao walionao jua, ndiyo! hekima ni ulinzi kama ilivyo pesa lakini ubora wa maarifa ni kwamba Hekima humhifadhi yeye aliyo nayo. (Mhubiri 7:11-12, Mithali 8:11).

This is my prayer for you today;
Mwenyezi Mungu akufanikishe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo (3 Yohana 1:2), huku ukijua kuwa ni baraka ya Mungu [ambalo ni Neno lake kwako] ndio itajirishayo (Mithali 10:22) na nguvu za kukufanya uwe tajiri zina yeye Bwana (Kumb. 8:18). Kwa hivyo usiache kamwe kumwamini BWANA Yesu Kristo aliye Hekima yako, hakika utafanikiwa katika maisha yako yote. Baraka ya BWANA ya kukufanikisha iwe nawe siku zote za maisha yako katika jina la Yesu Kristo, amina.

1 comment: