#ASILI YA MUNGU HAITAPATIKANA KWAKO DHAMBI IKIKUTAWALA

     Asili ya Mungu haitakuwa kwako ukiwa mdhambi hata zile kinga juu ya maisha yako kupitia roho wake Mungu hazitakuwa kwako, unaona saa nyingine katika mapito na majaribu yako wawezadhani kuwa Mungu yuko nawe na kumbe hayuko unakuwa mtupu kama ulivyozaliwa pasipo ulinzi. Hivyo yatupasa kukiri dhambi zetu na kumuomba Mungu aturehemu ili tufanyike wapya. Waamuzi 5:8 inazungumzia wana wa Israeli walipochagua miungu mingine Bwana hakuwa nao tena kwa maana hata katika vita na maadui hata kule kuwa na jeshi na silaha nyingi haikuonekana kuwa ni kitu. Joshua 5:12; inasema;”Ndipo ile maana ikakomaa siku ya pili yake, baada ya wao kuyala mazao ya nchi; na hao wana waisraeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika vilima vya nchi ya kaanani mwaka huo”. Kuna gharama tusipotii maagizo waweza ishi lakini pasipo kibali tena kwa Mungu kama cha awali, na kama utashupaza shingo kwa kutokiri na kutubia uovu shida itakuwa kwako daima, ndio maana wana waisraeli waliyotamani mazao ya nchi na kuidharau mana ambayo kwa miaka zaidi ya arobaini iliwafanya wawe hai jangwani Mungu akaiondoa kwao na hata mazao ya nchi waliyoyatamani yakapatikana kwao kwa shida. Anachoanzisha Mungu wache yeye amalize tusikengeuke na kuchanganya na vya dunia gharama ni kubwa sana wawezaona siyo shida lakini kiuhalisia ni shida ukikumbuka ulikotoka.

Usiruhusu kitu kiingilie mpango wa Mungu ndani yako. Nijuacho ni kwamba zijapo taabu, dhiki, shida na mateso sisi ni washindi katika kristo kama tu tukiutafuta utakatifu wake kila dakika kila saa. Mwanzo 3:7; inasema “wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua ya kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo”. Kutoka mwanzo twajifunza kwa habari ya Adam na Hawa siku zote walikuwa walivyo lakini siku walipotenda dhambi na kuasi maagizo ya Mungu ndipo walipotambua tofauti ndani yao iliyosababishwa na kutokukiri makosa, na baada ya kutafuta uso wa Mungu ili kukiri dhambi na kutubia makosa yao wao wakaona si shida wakajizuia na kujificha kwa majani na nguo, na kumbe swala si kuficha uovu bali kukiri na kutubia tufanywe wapya na ndivyo ilivyo hata kwa wakristo wa leo hatuombi kusamehewa ila tunatafuta namna ya kuonyesha kuwa dhambi tuzitendazo si dhambi.

Najifunza jinsi ya kuwa mwana wa Mungu kweli katika kitabu cha ufunuo 21:7-8, kwa kutokutenda yale yanayohesabiwa kuwa matokeo yake ni kwenda jehanamu. Lakini ndugu mkristo mwenzangu bado hujachelewa kiri maovu na dhambi zako mbele za Mungu leo na utubu ili usamehewe yeye ni mwingi wa huruma na anasamehe dhambi. Najifunza tena katika kitabu cha mwanzo 3:21 baada ya Adam na Hawa kukiri dhambi zao na jinsi ilivyotokea katika bustani, Mungu wetu aliye mwingi wa rehema akachinja mnyama na kuwafanyia ngozi akawavika ili kuwakinga na dhambi, tendo ambalo Yesu wa Nazareti alilikamilisha kwa kufa kwake msalabani damu yake iliyomwagika imefanyika utakaso kamili na wa milele wa kuzifanya upya dhamiri zetu katika agano lake jipya lililobora kuliko la kale ambapo pamoja na watu kutakaswa na damu ya wanyama haikutesheleza wao kufanywa upya dhamiri zao na kudumu katika njia za Mungu na kuyatenda mapenzi yake.

Tuenende katika kweli na kutenda mema na kushika na kuzitii amri za Mungu ili asili yake iwe ndani yetu tuwe na wasifu wa kristo hata ufalme wa giza utujue kuwa sisi ni wana wa nuru kweli (Matendo 19:11-17), Amina.

No comments:

Post a Comment