#NJIA YA BWANA

Mch. Daniel mwana wa Moses Kulola ~ EAGT @Lumala-Mwanza
Mithali 14:12 inasema; “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”. Iko njia ina maana ile namna ya kuishi kwa mtu; vile mwanadamu anavyoenenda. Namna unavyoishi unaweza kuona ni sawa kumbe ndani yake ni mauti inakuvuta.
Biblia takatifu katika Mwanzo 6:2,5 inasema pia; “2’Wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri, wakajitwalia wake wowote waliowachagua. 5’BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwandamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya siku zote”. Siku zote ukiamua kitu, mbaya zaidi kiwe kila kunachokuvuta katika uovu, kurejezwa sio rahisi kabisa, kwa maana sababu ya kuamua kwako yaweza kuwa uliona ni chema hivyo kukiacha si rahisi sana.
Mathayo 7:13; “ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo”. Mtu yeyote anayetaka kupita njia nyembamba amejinyima mengi, kwa maana njia hiyo ni ya kujinyima mengi sana. Mtu yeyote aliye na shida ni kwa sababu ya mambo mengi ambayo sehemu kubwa ni yeye wenyewe anakuwa amesababisha. Mengi ya mavuno ama matunda uyavunayo ni sababu ya yale uliyoyapanda mwenyewe.
Waamuzi 13:4-5; “Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi, kwani tazama utachukua mimba nawe utamzaa mtoto mwanaume na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti” na waamuzi 13:13-14 inasema: “Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, katika haya yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari. Asile kitu chochote kitokacho katika zabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu chochote kilichonajisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze”. Unaona mnadhiri wa Mungu siku zote ni mtu aliyetengwa na Mungu kwa kazi maalumu, hivyo Mungu hapendi kuchakachuliwa kwa kitu alichokiandaa maalumu kabisa, kwa maana safari ya mbinguni si ya wasindikizaji kama wachafu, waovu na wenye dhambi bali wale wenye tiketi ya kuingia huko. Umeokoka kwa neema ya Mungu, wewe ni mtu maalumu sana kwa Bwana hivyo itambue njia yake na uishi katika hiyo, na ndio maana Mungu anatuasa katika Biblia - 2 Timotheo 2:22 akisema; "Lakini zikimbie tamaa za ujanani, ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi".
Hivyo hatupaswi kuishi kama kibao kioneshacho mahali upaelekeapo hali chenyewe hakijawahi kufika pale wala kukaa mahali penyewe, na hii ni kweli kabisa hupaswi kuwaongoza watu kwa Yesu hali na wewe hujafika kwake, hushuhudiwi uko naye na unakaa naye, ila tunapaswa tuwe watu tunaoenenda na kukaa na Bwana nyakati zote kwa maana kama Zaburi 68:20 isemavyo “Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; na njia za kutoka mautini zina yeye YEHOVA Bwana”, na yeye Bwana hakika ndiye njia, kweli na uzima (Yohana 14:6). Barikiwa, Amina.

No comments:

Post a Comment