#ONGEZA UKUBWA WA MAHAKAMA YAKO ILI NAFSI YAKO IPONYWE NA ROHO YAKO IHUISHWE

Biblia inazungumzia uhusiano wa dhambi na sheria katika warumi 7 ya kwamba kuwepo kwa sheria kuliipa nafasi dhambi kutujaribu sisi; yaani ile sheria iliyonenwa au kutamkwa na kisha kuandikwa ilifanyiza kila namna ya kutuvuta ili tukwame kwayo. Na ndiyo maana mtume Paulo anasema asingelijua kutamani kama sheria isingelisema usitamani, kwani kwa kuwepo kwa sheria ya "usitamani" kulifanyaza ndani yake kila namna ya kutamani yaani kwa kutumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya kutamani ndani yake. Kuna msemo umezoeleka na wengi kwamba sheria imeweka ili ivunjwe, kwa kuwa kuwepo kwa sheria kunaipa dhambi nguvu na hii nijifunza sana kwa mtoto wangu mdogo kabisa kila nilipokuwa nikimkataza kutofanya kitendo fulani, yeye ndicho akazidi kukitenda na saa nyingine hata akiamka asubuhi akili yake inamfanya ananze nacho, yaani kile nilichomkataza ndicho alichovutwa kukitenda na kile kizuri alichokitenda sikumsemesha lolote bali sasa yeye kile kibaya kikawa kina Nguvu sana ndani yake, kwa maana nyingine nisingemfanyia sheria kile asingefungwa nacho, uhuru wake katika kile kitendo kibaya ulikuwa katika kutokumuwekea sheria au kumfungua. 
Hivyo sheria ilivuta dhambi ingawa sheria yenyewe ilikuwa ni njema na takatifu na hukumu ya mwili ikawepo na ndio maana mwili huu huitwa mwili wa dhambi, kwa maana mwili kama mwili hauwezi kuvutika katika jema wenyewe isipokuwa dhambini. Kwa hiyo kama vile hukumu isingekuwepo pasipo sheria vivyo hivyo bila sheria dhambi isingekuwa na nafasi yaani ingekuwa kama kitu kilichokufa, kwani kusingekuwa na kipimo cha ukosaji au usahihi katika jambo lolote lile hivyo hata mauti isingekuwa na nafasi.
Dhambi ilikuwa na nguvu kwa kule sheria kufunuliwa kwetu, ingawa sheria yenyewe ilikuwa ni njema na takatifu, na ndio maana biblia inasema Nguvu ya dhambi ni sheria. Na ndio maana kabla ya torati ya Musa, Mungu ndiye aliyejua kipimo cha usahihi katika kila jambo na kiwango cha utakatifu duniani, na hata wanadamu walioishi kabla ya torati waliishi pasipo kufunuliwa haki na hukumu za Mungu kila mwanadamu alitenda vile ilivyompendeza machoni mwake; na hata walipokosa sana biblia inaelezea kuna sehemu Mungu alishusha gharika wakati wa Nuhu na moto wakati wa Noa kwani hakuna aliyehisi kuwa hayuko sahihi katika matendo yake, kila mwanadamu alijihesabia haki mwenyewe ndipo Mungu mwenye kipimo cha haki kabla sheria haijashuka duniani aliwaadhibu wakosaji waliotukuka katika maovu yao, ambao walifanya maovu yaliyokuwa chukizo kuu mbele za Mungu. Lakini sheria iliposhuka tu yeyote ambayo hakuitenda au kuitii sheria kwa kifungu hicho hicho alihukumiwa, kwa maana ilikwisha funuliwa kwao.
Lakini sasa ashukuliwe Mwenyezi Mungu tunayo neema kuu katika Kristo Yesu, ambayo kwa upendo mkuu umetuondoa katika vifungo vya torati kwa miili yetu kufa pamoja naye Yesu kristo ili ile dhambi iliyoifanya mauti kuwa na Nguvu juu ya miili hii isiwe na Nguvu juu yetu tena wala sisi kuizalia mauti matunda, bali sasa neema hiyo imetuhuisha roho zetu ili tuweze kumzalia Mungu matunda yaliyo mema na ya haki katika Roho wake Mtakatifu; Kwa maana Roho mtakatifu amekuwa mshauri wetu wa ajabu na kutufanya tutubie kila tutendapo maovu yaani ametufahamisha na anazidi kutufahamisha yaliyo mema na mabaya na tunayopaswa kutenda na kutoyatenda; Hivyo ndugu tamani kuwa na Roho Mtakatifu kupitia Yesu Kristo ili uweze kuongozwa kwa Roho, tanua mahamaka yako ili roho yako ihuishwe zaidi na zaidi na nafsi yako iponywe kupitia kusoma Neno lake Mungu takatifu kwa maana zidi unavyomjua ndiyo unavyozidi kuchukua mabaya na kuyapenda mema; na nasema ni mahakama kwa sababu vile unvyolijua Neno lake ndivyo unavyoongeza ukubwa wa eneo lako la kuponywa nafsi na kuhuishwa katika roho, na ndio maana pia biblia inasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa na maarifa yanakosekana kwa kutokuwa na ufahamu wa Neno. Kujua Neno inakufanya kila unapojaribiwa kwenda njia mbaya ndiyo muda huo Roho mtakatifu akuhukumuvyo kwamba usitende jambo hilo kwani ni baya hali anakuponya nafsi yako na roho yako kuhuishwa. Hivyo agano la Mungu wetu Bwana Yesu ni bora zaidi kwa kuwa linakazia lile agano la kale kwa kushughurikia madhaifu yetu rohoni (yaani kuihukumu dhambi rohoni mwetu kabla hata haijathihirika mwilini, hivyo ni mwanadamu mwenyewe apende kuanguka dhambini) kwani hatuhukumiwi moja kwa moja matendo ya miili yetu bali chanzo cha matendo hayo ambayo huanza rohoni.
Mpokee Yesu leo ili ufunguke kupitia Roho wake mtakatifu, Amina.

No comments:

Post a Comment