#DHAMIRI YAKO YAMTEGEMEA YESU WA NAZARETI ILI KUTENDA MEMA

1 Timotheo 3:9 inatusisitiza ya kwamba tuishike siri ya imani katika dhamiri safi.

Dhamiri maana yake ni ule uwezo wa fikra zetu kutofautisha yale yaliyo mema na mabaya na kutenda sawia. Hivyo dhamiri ni namna ya fikra kuweza kutofautisha au kufanya maamuzi sawasawa yale mtu ayadhaniayo kuwa ni mema au mabaya. Dhamiri ina muhimu na ni msaada kwetu ikiwa na msukumo wa Roho mtakatifu kwani hututaka sisi kufanya mema na kuacha mabaya yaani yale tu mtu ayafikiriayo kuwa ni mema ambayo kweli ndiyo hivyo huyatenda hayo. Wengine hufananisha dhamiri ya mtu ni kama saa iliyosetiwa sawasawa ili
kutekeleza kusudio muhimu, lakini kama ikisetiwa vibaya (na maana kama haijulikani ndani yako lipi ni jema na lipi ni baya), dhamiri yako itakuelekeza katika mapotofu, yaani kufanya maamuzi yaliyo changanyika au yasiyofaa. Hivyo dhamiri ili iwe safi inategemea msukumo wa ndani wa Roho mtakatifu ambapo mtu kule kuweza kuutambua na kuunganishwa na fikra zake kutamuwezesha kutenda mema siku zote.


Dhamiri siku zote haiwezi kuwa mwongozo wa kufuata pasipo kristo, Mtume Paulo anasema amemtumikia Mungu katika dhamiri safi katika maisha yake yote (Matendo 23:1), hata alipokuwa anawaua wanaoliitia jina la Yesu (Matendo 26:9-11) alijua anatenda mapenzi ya Mungu kwa sababu alifikiria (dhamiri yake ilimuongoza) kwamba anatakiwa kilipinga jina la Yesu, hivyo dhamiri yake ilifanya kazi sawasawa lakini ilisetiwa isivyo sawasawa, kwa hiyo hata sisi tunapaswa tujiulize je’ vile tunavyodhani ni sahihi yaani yale mema na mabaya tudhaniavyo ndivyo ilivyo kwa Mungu? Na je maamuzi yetu juu ya mema na mabaya yanasimamia katika Kweli halisi ya Mungu?, yaani dhamiri zetu zimesetiwa sawasawa? Jiulize ndugu.


Ni kwa namna gani dhamiri inakuwa safi, biblia katika Warumi 3:23 inasema wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, sasa ni vipi na ni kwa namna gani dhamiri zetu zinakuwa safi mbele za Mungu?. Katika agano la kale sadaka za kuteketeza na matoleo havikutosheleza (Waebrania 9:9 na 10:1-4), kwa hivyo ni damu ya Yesu pekee yake katika agano jipya ndio iwezayo kusafisha Dhamiri ya mtu (1 petro 3:21). Kwa hiyo basi katika ubatizo tunafanywa wapya katika dhamiri zetu yaani kama ni saa inakuwa imesetiwa sawasawa, huku tukiamini damu ya Yesu ndiyo ioshayo dhambi zetu (Matendo 2:38 na 22:16).


Na je’ ni kwa jinsi gani dhamiri inakuwa na mtizamo ule ule, dhamiri safi inatunzwaje na utii wetu katika matakwa ya Mungu. Kumbuka ya kuwa tusipotenda lile tunalofahamu kuwa ni jema ni sawa na kutenda dhambi (Yakobo 4:17) vile vile kushindwa kutokufanya yale yaliyomabaya ni dhambi pia. Kufanya kwa utakatifu na ukweli utokao kwa Mungu inatujengea kuwa na dhamiri safi (2 wakorintho 1:12), kule kufanya lililojema na la haki kiukweli kunaunda ujasiri ndani yetu. Kwa hiyo vile unavyofanya yaliyo mema zaidi na zaidi ndivyo uwezavyo kujitenga na yale yaliyo mabaya, na ndivyo bora na safi dhamiri yako itakavyokuwa ndani yako. Kwa neema ya Mungu hata waliokubuhu katika dhambi wanaweza kusafishwa dhamiri zao kupitia imani katika kristo yesu wanaweza kufanywa dhamiri zao kuwa safi lakini ujue pia kunauwezekano wa kuharibu dhamiri zetu.


Kwa namna nyingi dhamiri zetu zinaweza kuharibiwa; (i)kwa kutokuitii dhamiri ambapo ni kutenda dhambi (Warumi 14:22-23), (ii)kwa kuichakachua dhamiri ambapo inapelekea kutokuwa na imani (1 Timotheo 1:15), na pia (iii)kwa kuichoma dhamiri, hii inapelekea kutokukuyakubali mafundisho ya Mungu na kutoamini tena (1 Timotheo 4:1-2). Kuiacha dhamiri au kuiharibu ni hatari sana, kwa sababu dhamiri iliyo na hatia inapelekea mtu kuwa na dhamiri ngumu yaani kama usemi usemavyo sikio la kufa halisikii dawa na dhamiri inakuwa hivyo kwa hiyo ule muunganiko na Mungu hauwepo tena mfano; mtu akiwa na dhamiri ngumu haoni haja hata ya kwenda kanisani, hudumani wala hahukumiwi moyoni mwake maana amepoteza ile signal ya Roho mtakatifu anakuwa yupo yupo tu kule kwa kwenda haendi na kule anakopaswa asiende yeye ndio anaenda (Waebrania 10:25). Hii inamfanya awe mgumu hata kutenda yaliyo ya haki katika maeneo mengine pia ya maisha yake, na kama nilivyosema dhamiri ngumu inapelekea moyo wa kutokuamini (Waebrania 3:12) kwa hiyo ule uwongo mkuu wa dhambi na kutokutenda mema unafanya mtu kuwa na moyo mgumu, Na moyo mgumu humfanya mtu kuanza kuuliza hata kile alichokiamini mwanzoni.


Ndugu tunaweza kuomba pamoja maandiko yaliyo katika biblia - waebrania 13:18; ya kwamba “tuna imani kuwa tuna dhamiri safi na katika kila kitu tunapenda kufanya yaliyosawa daima, Amina”.


Mtume Paulo anasema nakushukuru Mungu ambaye ninakutumikia kwa dhamiri safi (2 Timotheo 1:3), kama sio na dhamiri zetu hazijakuwa ngumu bado ya kwamba hatutasikia, hivyo tunapaswa kumwendea mwana wa Mungu(Yesu kristo) ili asafishe dhamiri zetu kwa damu yake, na pia turirejee neno la Mungu ili tupatekufahamu sawia kwamba yapi kweli ni mema na mabaya mbele za Mungu. Karibu katika familia ya Mungu kupitia makutaniko ya mara kwa mara popote wanapoliitia jina la Kristo Yesu ili kumuomba Mungu atuwezeshaye kuwa na dhamiri safi daima, Je’ kinini kinakuzuia usimtumikie Mungu katika dhamiri safi leo?.

http://www.slideshare.net/Recknald/depend-on-jesus-of-nazareth-man-is-a-mere-vapour

No comments:

Post a Comment