#KUUKOMBOA WAKATI KWA KUWA NA UJASIRI KATIKA MAAMUZI NA IMANI ISIYOTIKISIKA

  Matendo ya Mitume 7:22-35; Neno linasema; 22 Musa alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa mashuhuri kwa maneno na matendo. 23 Alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kwenda kuwaona ndugu zake Waisraeli. 24 Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda kumwokoa, na kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri. 25 (Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo.) 26 Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha, akisema: Ninyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya ninyi kwa ninyi? 27 Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu? 28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana? 29 Baada ya kusikia hayo Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili. 30 Miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Musa katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai. 31 Mose alistaajabu sana kuona jambo hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana: 32 Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo! Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi. 33 Bwana akamwambia: Vua viatu vyako maana hapa unaposimama ni mahali patakatifu. 34 Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri. Nimesikia kilio chao,nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa,nitakutuma Misri. 35 Huyu Musa ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa waliposema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu? Kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu alimtuma Musa huyo awe kiongozi na mkombozi. 36 Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa muda wa miaka arobaini.
Sehemu A: Bwana Yesu asifiwe tumepewa ufahamu utumie upate kufahamu na kujawa na maarifa na Hekima ya Mungu. Katika hili Neno tunaona Musa alipofikisha miaka 40 aliazimia kuwasaidia ndugu zake kutokana na kibali alichopewa na Mungu katikati ya waisraeli waliokuwa utumwani Misri kilichomfanya akubalike katika familia na utawala wa farao. Ule mzigo ndani yako juu ya ndugu ndio uliompelekea yeye kuazimia na kufanyika njia ya Mungu kuzungumza na wana wa Israeli waliokuwa utumwani. Lakini dhidi Musa alivyoonyesha kuugua kwake moyoni dhidi ya mateso yao na kuonewa kwao, neno la Mungu linasema ule mistari wa 27 kwamba yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Musa kando akisema: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu?.  Biblia inatuambia maneno ya Yule mtu yalimshitua sana Musa na kumfanya akimbilie nchi ya midiani. Yawezekana aliyemtisha Musa alijua hakika Musa ndiye Kiongozi na mwamuzi wao kwani twajua shetani wa mtu ni mtu, na shetani humtumia yoyote yule na pengine alijua Musa anaanza kazi yake ambayo kwa hiyo aliletwa duniani, akamtisha. Hofu na woga ni maadui wakubwa wa Imani kile ukionacho kwa macho ya rohoni au ushuhudiwacho moyoni shikilia shetani siku zote hupinga penye anguko lake. Ukiruhusu woga au hofu utawale maono yako hupotea na gharama ni kubwa. Yesu alipoulizwa eti wewe ni mfalme wa Wayahudi akasema wewe wasema, kwani yesu alijua inajulikana hivyo na alizidi kukiri hivyo. Lakini Musa alihofu baada maulizo ya vitisho kwa maana alidhani kwamba Waisraeli wenzake wajua kwamba Mungu ameweka mzigo ndani yake juu yao, Saa ingine yafaa kushikilia kile kilichojulikana ndani yako hata kama utapingwa, kurudi nyuma ni ishara ya kushindwa na kutokuwa na ujasiri. Ilimchukua Musa miaka 40 tena tangu alipokimbilia nchi ya midiani si kwa kumtafuta Mungu bali kwa hofu ya ule utisho na akaanza kufanya mambo mengine tofauti na ule wito uliojengeka moyoni kwa mzigo mkuu tangu alipokuwa na umri wa miaka 40, hofu na woga ilimsababishia gharama ya miaka 40 kusota ugenini pasipo kutimiza wito wa roho ambao ulikuwepo tangu alipokusudia na kuazimia kuwa msaada kwa wengine. Nasema ni hofu na woga kwa sababu hata Malaika wa Bwana alipomtokea katika mwali wa moto kumtaka arudi misri kuwaokoa wana waisraeli kutoka utumwani bado Musa alidai nitasema nimetumwa  na nani?, nitafanyaje ili waniamini kwamba nimetumwa?, kwa maana nyingine hofu ilikuwa bado ingalimo kwamba hawa ndugu niliokusudia kuwasaidia hawakuamini wataniamini tena?. Mpaka alipopewa ishara za Uungu za kuwaonyesha na pia akapewa na msaidizi Aaroni.  Kwa hiyo ile Imani ya kwamba Mungu anataka kumtumia yeye kuwakomboa na kuwaongoza ilikuwa dhabiti tangu alipokuwa na miaka 40, hivyo hata katika yale maulizo yao, Je ni nani amekufanya wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu? Hekima ya Mungu ingesimama kama tu pasingekuwa na hofu na woga, ndio maana pia Neno linasema mkisimamishwa mbele ya baraza msifikiri fikiri mtasema nini Bwana asema nitawajaza neno kupitia Roho mtakatifu. Kutambuliwa au kutokutambuliwa kwako sio kigezo chakutumika au kutokutumika na Mungu na pia uwe unatambua au humtambui Mungu aliyekutuma sio kigezo kuwa wewe sio chombo cha BWANA. Mungu humtumia yeyote amtakaye kwa wakati wake aidha anajulikana au hajulikani au aidha anamjua Mungu au hamjui, Kizuri au kisichofaa, chema au kibaya, cha heshima au chakudharauliwa vyote ni vyombo vyake vinavyomfaa Mungu kwa kazi yake kwa majira yake.
Neno linasema Imani ni kuwa na hakika juu ya mambo yatarajiwayo na ni bayana ya mambo ambayo hayajatokea bado, twajifunza kung’ang’ana na Imani kwani mwenye haki wa Mungu ataishi kwa imani na akisitasita neno linasema Bwana Mungu hata kuwa na haja naye tena. Hebu fikiria kwa habari ya Musa miaka 40 kutoka nje ya mstari je, hii si gharama?. Wajua maono na malengo uliyonayo, utafikaje kwa wakati sahihi ulioamuliwa pasipo Imani na ujasiri wa yale uyakusudiayo kutenda?. Kwani twajua wakatishaji tamaa wapo na wakwazao pia ili ya kwamba ushindi uwe mkuu kwa maana utahesabiwaje ushindi hali huna mshindani? Na kipimo cha kupima yupi yupo juu ni kuwepo na washindwaji wa chini. Hivyo komboa wakati kwa kuwa na ujasiri katika maamuzi na imani isiyotikisika.
Na pia kaa ukijua ya kwamba ni mengi waweza kuyafanikisha pale tu Mungu akiwa nawe kuliko ukiwa wewe kama wewe. Musa tangu utoto hadi miaka 40 alipoanza kupata mzigo wa kuwasaidia wana waisraeli hakuenenda katika wito huu baada ya utisho, hofu na woga bali alikimbilia Midiani na huko ikamchukua miaka 40 tena, hakuna makubwa aliyoyafanikisha maishani mwake hadi alipofikisha miaka 80 zaidi ya i) kumuua Mmsiri ii) kumuoa Siphora iii) kupata mtoto wa kiume, ambayo hayo kama mafanikio yake yameandikwa katika sura (chapters) 7 za Biblia. Lakini pale alipoingia kikamilifu katika wito wa Mungu alifanikisha mengi zaidi ya sura (chapters) 37 za Biblia na pia aliweza kutusaidia wakristo wa sasa kwa kuandika Torati yenye vitabu vitano (5) ambayo kwa hiyo tumeweza kumjua Mungu na kuzitambua njia na hukumu zake Mungu.
Kwa hivyo hii ni uthibitisho kuwa Mtu ukiwa na Mungu na huko Roho mtakatifu akikuongoza unatenda na kufanikisha mengi zaidi kuliko pale ukiwa wewe pasipo Roho mtakatifu.

Sehemu B: WAWEZA SAIDIKA NA USIYEMJUA KWANI MUNGU NJIA ZAKE HAZICHUNGUZIKI
Jina la Bwana lihimidiwe!, Kwa upande wa pili wa neno hili twajifunza usimtende mabaya mtu usiyemjua wala kumdharau kwa maana kama neno lisemavyo wengine walifanya hivyo kumbe walifukuza malaika. Mungu hutuma msaada na kubariki kupitia wanadamu hakuna mtu aliyepokea baraka isipokuwa kupitia wanadamu, Mungu mwenyewe akiri kupitia kinywa chako nitanena na kupitia mikono yako nitabariki. Usimkwaze usiyemjua usijeukapoteza muujiza wako, Mungu hutuma msaidizi kwa wakati sahihi na uliopangwa.
Tunaona wana wa Israeli kwa miaka zaidi ya 300 walikuwa utumwani Mungu alifunulia Musa ili kwa huyo kwa kuambatana naye wapate wokovu lakini alipoanza kufanya yaliyokusudiwa na Mungu hawakuona kwamba yeye ni msaada. Ikawachukua miaka 40 kupitia shida ileile utumwani kwa kukataa msaada walikuwa wanauhitaji, swala ni kwamba hawakutambua kuwa ndiye msaada wao. Ipo gharama katika kupinga pinga kwa maana wapo waliopinga msaada au baraka walioihitaji pasipo kutambua. Katika unyenyekevu kuna Faida kubwa na dhawabu pia kwani waweza karibisha Baraka au msaada nyumbani kwako. Malaika huwaelekea wenye uhitaji na uhitaji husomeka moyoni na sio usoni au jinsi mtu alivyo. Unajua Musa alibeba nguvu za Mungu lakini kutokana na kupinga kwao akaenda kukaa nazo sehemu isiyosahihi (midiani) kwa miaka 40 huku akifanya mambo mengine kabisa tofauti na wito uliotengeza mzigo ndani yake juu ya ndugu na kuwaacha wana waisraeli wote pasipo nguvu za Mungu za kuwasaidia kutoka kifungoni.
  Wanawaisraeli wasingempinga Musa na kuambatana naye katika imani aliyokuwa nayo kusingekuwapo nguvu za wao kushikiliwa utumwani, Wao walilaani na kulaumu ya kwamba Musa ndiyo aliyekuwa anawataabisha na hiyo iliwachukuwa muda mrefu kufika nchi ya ahadi. Kwa maana hata walipotolewa misri jangwani waliendelea na lawama hiyo na pia kwa kutokusadiki kwao matendo makuu ya Mungu iliwagharimu miaka mingine 40. Kama Mungu aliona Musa ndiye alifaa katika ukombozi huo na kuwaongoza, wanadamu ni nani hata waseme hapana.

Mungu anatoa msaada kupitia mwanadamu, kwa kuzuia kwako unajizuilia Baraka zilizoelekezwa kwako kwa maana kupitia binadamu mwenzako Mungu atashusha Baraka. Imani ya matendo ni pamoja na kumwamini aliyetumwa na Bwana, kuna dhawabu katika kumwamini roho wa Mungu, Mti  au jiwe mara nyingi msaada hauko katika hayo bali mwanadamu na ndio maana hata Nabii eliya alipobaki mwenyewe wengine manabii wakiwa wameuawa Mungu alisema nimejisazia watu 7,000 wenye utii ambao nitawatumia pamoja na yeye kupata msaada.Amina!

No comments:

Post a Comment