#TUBEBEANE MIZIGO SISI KWA SISI (WAGALATIA 6:2)

Danieli 12:3; inasema “na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga, na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele”, soma pia Yakobo 5:19-20 na Petro wa kwanza 4:8. Kuna faida katika kuwasaidia waliolemewa na mizigo kuwaelekeza katika njia ya haki. Biblia pia katika Warumi 15:1-3 inasema; "basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake apate wema ajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe bali kama ilivyoandikwa; "malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi"”. 

Neno linatusisitiza kuchukua udhaifu wao wasio na nguvu ili wapate wema na kujengwa kiimani kwa sisi kuwa sehemu katika shida zao na matatizo yao kwa maana huo wema nasi tutaupata na kujengwa pia. Biblia katika kitabu cha Ayubu 1:5 kinatufundisha namna ya kusimama kwa ajili ya wengine kubeba mizigo ya ndugu, marafiki, majirani, wajane, yatima, familia na wengineo wasio jiweza, kwa habari ya Ayubu biblia inasema;”Basi ilikuwa hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia,Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa ; kwani alisema, Yamkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi na kumkufuru Mungu mioyoni mwao, ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote". Hivyo mizigo ya wengine tuwasaidiao katika kristo tusichoke wala kukoma mpaka furaha zao zitapowarejea tena na amani ya roho zao ili wapate wema na kujengwa na Bwana nasisi pia.