#MVUTE YESU KRISTO KWAKO

Yale uyatafakariyo kwa kina kutoka ndani kabisa ya kirindi cha moyo wako yaani lilo neno la Mungu ambalo kila wakati unakuwa ukilitafakari, ukilifikiria na kumshangaa Mungu kwa hilo jinsi alivyo wa ajabu na mkuu sana, ni kwa hilo ndipo utamwona Mungu na atajidhihirisha kwako na hiyo ndiyo kweli itakayo kuweka huru kabisa, na jambo hili ndilo liwafanyalo wanadamu kuwa na hofu ya Mungu na moyo wa uchaji katika kristo. Udhihirisho wa Mungu kwako ni mpaka umtafakari na kumfikiri yeye kwa kina, kupitia neno lake, kwa sala, kwa sifa na kwa kuabudu na lile jawabu ulipatalo ndio udhihirisho wa Mungu kwako katika muda ule na ule ujumbe kutoka kwa mtumwa wa Bwana.
Hebu kwa sekunde kadhaa fikiri kwa kina sana, na najua kwa Bwana unaweza pata ufunuo kwamba ilikuwajekuwaje;
Je Zakaria akiwa hekaluni alikuwa anatafakari nini kwa kina ile kabla tu Malaika Gabrieli hajamtokea? (Luka 1:5-16)
Je Bikira Mariamu alikuwa anatafakari nini kwa kina ile kabla tu Malaika Gabrieli hajamtokea? (Luka 1:26-35)
Je Wachungaji walikuwa wakitafakari nini kwa kina pale walipokuwa wanachunga mifugo kwa zamu ile kabla tu Malaika wa Bwana hajawatokea? (Luka 2:8-15)
 Je Gideoni alikuwa akitafari nini kwa kina ile kabla tu Malaika wa Bwana hajamtokea pale kwenye mti wa mwaloni? (Waamuzi 6:11-13)
Je Mama yake Samsoni alikuwa akitafari nini kwa kina ile kabla tu Malaika wa Bwana hajamtokea? (Waamuzi 13:2-3)
Je Musa alikuwa akitafakari nini kwa kina ile kabla tu hajaona Malaika wa Bwana kwa njia ya kijiti kinachowaka pasipo kuteketea na Bwana kuzungumza naye? (Kutoka 3:1-10)
Je Joshua alikuwa akitafakari nini kwa kina ile kabla tu hajamuona Malaika wa Bwana na upanga alipokuwa akitaka kwenda kuushambulia mji wa Yeriko? (Joshua 5:13-15; 6:1-2)
Je Eliya alikuwa akitafakari nini kwa kina ile kabla tu Bwana kujidhihirisha kwake kule mapangoni? (1 Wafalme 19: 4-8)
Je Kornelio alikuwa akitafakari nini kwa kina ile kabla tu Malaika wa Bwana hajamtokea mchana kweupe? (Matendo 10: 1-8)
Hebu fikiri, Je mitume walikuwa wakitafakari nini kwa kina mle ndani ile siku ya pentekoste ile kabla tu Mungu hajajidhirisha kwao kwa kuwavuvio Roho mtakatifu kwa nguvu? (Matendo 1: 14; 2:1-4)
Na je hebu fikiri kwa kina mwenyewe wale watu wawili waliokuwa wanatokea Yerusalemu walikuwa wanafikiria nini na wanatafakari nini hasa na kushirikishana nini kuhusu Yesu kulichowapa majonzi na mzigo mkubwa moyoni mwao kwa kiasi ambacho mpaka wakahisi kuwaka moyoni mwao pasipokujua Yesu amefufuka na alikuwa ameambatana nao na ndiye aliyekwenda nao kula pamoja na akafanya ishara ya meza ya Bwana mbele yao. (Luka 24:13-32)
Hebu tu wewe mwenyewe fikiri kwa kina kuna uhusiano mkubwa kati ya yale tuyafikiriyo na tuyatafakariyo iwe kwa Neno kulisoma au kulitafakari, kwa sala, kwa kusifu na kwa kuabudu na yale yajidhihirishayo kwako baadaye yaani ile tu baada ya mawazo uliyonayo katika fahamu zako yatokayo moyoni mwako. Kutokana na mifano ya hapo juu hawa watu wa Mungu ile kabla tu Mungu hajajidhihirisha kwao, nikwambie tu hawakuwa wanarukaruka ama kuchezacheza tu au kufikiria upuuzi bali walikuwa katika kufikiri na kutafakari yaliyo ya Mungu na hayo ndiyo yaliwapeleka katika uwepo mkuu uliokuwa unawapeleka ulimwengu mwingine wa rohoni yaani walikuwa katika roho kwa mambo ya rohoni haswa na sio katika mwili wa nyama kwa kiasi ambacho kulikuwa hakuna namna ya Mungu kutoweza kuvutika kwao ndani ya moyo yao na hata kujidhihirisha kwao kwa njia ya malaika zake. Unajua ni mshangao na saa nyingine inashitua sana kwa wengi pale yale tuyafikiriyo na kuyatafakari kutokea mara yaani wakati huo huo ukiwa bado katika tafakari, inakufanya ushuke na kububujika moyoni kwa namna ambayo uwepo wa jawabu lako huwa ni utukufu mkuu wa Mungu kwako, na huo ndio ukawaida wa uwepo wa Mungu tunaopaswa kuwa nao watoto wa Mungu katika Bwana kwa sala, dua na tafakari zetu kumbuka Henoko alitembea na Mungu miaka 300.

Kwa hiyo ni wewe ndiye unayepaswa kumvuta Mungu kwa karibu kwako kupitia jina la Yesu Kristo kwa kumfikiri yeye, kutamani kuwa naye kila wakati, kuishi naye akiwa ndani yako, hivyo ndivyo ukaribu ule muunganiko na Mungu uundavyo kupitia roho mtakatifu. Yale uyafikiriayo katika fahamu zako na yale yaliyo moyoni mwako ya wazi mbele za Mungu hakuna kinachoweza kufichika kwake siku zote yeye hujidhihirihsa kwa wakati wake. Tamani kuwa naye, mfikiri yeye usiku na mchana na litafakari Neno lake Mungu, Yesu kamwe hata kuangusha na hakika roho mtakatifu atajidhihirisha katika maisha yako sio kwa asilimia fulani tu bali mzima kabisa kwa sababu ni Mungu, Amina.

No comments:

Post a Comment