#UPENDO WA KWELI HUSHINDA MABAYA YOTE


Mtegemee Yesu wa Nazareti kwa kuwa upendo wake ni wa hakika na kweli, na yeye ni mfano kwetu wa kufuata na kuigwa yale maisha yake duniani (yaani Maisha ya Yesu wa Nazareti) kwa maana utakatifu wote hupatikana katika yeye. Na ndio maana hata Biblia katika Yohana wa kwanza 4:8 inasema MUNGU ni PENDO; na siku zote upendo wa kweli hushinda maumivu, shida, dhiki, dhihaka, taabu, ubinafsi, upweke, karaha, manyanyaso, mateso, hila, lawama, laana na mabaya mengineyo yote (1 wakorintho 13: 1-13).

Isaya 53:2-5 inasema; Yeye (Yesu wa Nazareti) ni kama mzizi katika nchi kavu, alidharauliwa na kukataliwa na watu kwa ajili yangu na wewe, mtu wa huzuni nyingi na ajuaye sikitiko hiyo yote kwa ajili yangu mimi na wewe, alidhauraliwa kiasi cha kuonekana si kitu kwa ajili yangu mimi na wewe, aligongelewa misumari mikononi na miguuni, alivikwa taji ya miba na kusokomewa katika fuvu lake kwa mwanzi, alipigwa mijeredi mpaka nyama zikanyofoka mwilini hii yote ni kwa ajili yangu mimi na wewe, Haikutosha pamoja na kuharibiwa vibaya na kuchubuliwa mwili wake kwa mateso makali bado alibebeshwa msalaba mzito na kuchapwa mijeredi kwa ajili ya dhambi zako na mimi na mkuki ubavuni alichomwa kwa ajili yangu mimi na wewe. Kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23), yeye alifanyika laana (Wagalatia 3:13) mpaka kifo cha msalaba ili kuizima nguvu ya mwovu shetani juu yetu na adhabu ya Amani yetu ilikuwa juu yake. Kwa damu yake pekee ya thamani na inayonena mema kuliko ya habili (Waebrania 12:24) lile deni letu la dhambi lilipwa pale msalabani, Kwa maana pamoja na mateso makali yote hayo pamoja na damu yake kumwagika hakumulaumu yeyote wala kulalamika mbele za Mungu Baba bali alisema Ee! Mungu wasamehe kwa maana hawalijui walitendalo. Pamoja na yote hayo aliyotendewa alivumilia mpaka mauti kwa ajili yangu mimi na wewe aliteswa sana mateso makali lakini kutokana na nguvu ya upendo ndani yake hata misumari, mkuki ubavuni, taji ya miba, mijeredi ya kurarua nyama na kuchubua, kuning’inizwa kwake msalabani, damu yote kutiririka ardhini (ili kubadili laana kuwa Baraka); vyote hivyo havikuonekana ni kitu kwake wala havikuweza kuutoa uhai wake hiyo yote ni kutokana na upendo mkuu aliokuwa nao na ndio maana Yohana 19:28-30 inasema hali akijua yote imekwisha na neno limetimia akasema nasikia kiu akapewa siki baada ya kuipokea akasema IMEKWISHA akainamisha kichwa, akaisalimu roho yake. 

Huu ni upendo wa kweli na wa ajabu sana aliokuwa nao juu yetu na aliouonyesha pale msalabani kwa kiasi ambacho hata na maumivu yote hayo yalishindwa na upendo huo. Hakika, hakuna aliyewahi kuonyesha upendo wa namna hiyo kama Yesu wa Nazareti, Ndio! Hakuna, Watu waweza kuwanao kwa wawapendao tu lakini kule kuwa na upendo mpaka kifo kwa wote yaani na maadui pia kwa wabaya na wazuri hakuna aliyewahi fanya kama yeye.

Hivyo tumtegemee Yesu wa Nazareti kwani hataacha miguu yetu isogezwe na atatulinda na mabaya yote (Zaburi 121:1-8). Nami naamini upendo wa kweli husitiri wingi wa dhambi (1 Petro 4:8), hivyo tumuombe Bwana Yesu wa Nazareti atuwezeshe nasi tuwe na upendo wa kweli kwa wote kwani pasipo yeye hatuwezi lolote na ni yeye tu aliyeshinda hivyo tuombe kushinda katika yeye katika vyote na tujifunze kumtii na kumnyenyekea kwa kuwa njia za haki na hukumu zina yeye, Amina.

No comments:

Post a Comment