#WATATU WALISULUBIWA PALE GOLGOTHA

Luka 23:39-43; Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini Yule wa pili akamjibu akamkemea akisema, wewe humuogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?. Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

Msalaba wa kukataliwa:
Yeye aliyekufa na dhambi zote alizokuwa nazo yule aliyemkebehi Yesu kristo pale msalabani, kwa maana pamoja na adhabu ya maovu yake hakutaka kusarenda kwa Yesu bali alimkebehi na Yesu hakuwa na haja naye isipokuwa alisema tu Ee Mungu wasamehe kwa sababu hawajui walitendalo. Yule mhalifu kwenye Luka 23:39 alimkebehi Yesu kama vile mtu asiye na uhitaji wala shida na Mungu hatimaye akafa na dhambi zake, na maneno aliyoyatoa ya kebehi yanawakilisha uadui walionao wengi kuhusu Yesu kristo wanashida, matatizo lakini hawamuamini kwamba ndio njia, kweli na uzima, na hii tu ni kwa sababu ya yeye Mungu kufanyika mwili na kukaa kwetu ile kufanyika mwili imekuwa shida kwao na ndio chanzo cha kutokuamini, Lakini kwetu tunaoamini ni upendo mkubwa na wa pekee aliouonyesha Mungu kwamba sisi ni wa thamani kwake, nawe amini sasa. Ona mtu upo kufani baada ya kuchagua neema yake Mungu kupitia Kristo unaona ni bora kuchagua kumkufuru mwana wa Mungu. Ni ngumu kufikiria vile kiumbe wa Mungu anavyomkataa Muumba wake kwa wakati wowote, lakini kuonyesha kumkataa hali yu kufani inashangaza zaidi na inaonesha jinsi mioyo ya wanadamu ilivyomigumu kuliko jiwe. Na ni katika msalaba huu huu wengi wamepotea na wengine wanazidi kupotea.

Msalaba wa Toba:
Yeye aliyekuwa na dhambi na akasulubiwa kwa maovu aliyoyatenda lakini akafa pasipo dhambi kwa maana yesu kristo alimuahidi kuwa naye peponi. Ni yule mhalifu wa pili ambaye yeye alitambua maovu yake na kukiri kwamba ni mkosaji na kuomba rehema mbele za Yesu kristo akapona na kuahidiwa uzima. Huyu ni yule kwenye Luka 23: 40-42, yeye alikuwa na mtizamo tofauti kabisa na alimkemea mhalifu mwenzako kwa kutokutambua njia ya kusamehewa makosa na dhambi, na akamwambia kwamba sisi tunapata tunayostahili ni kwa maovu yetu. Yeye hakumkebehi Kristo alimwona ni Bwana na sio tu mwanadamu wa kawaida na alimwomba Bwana Yesu amkumbuka akiingia katika ufalme wake na ikawa hivyo. Ni vema na muhimu mwanadamu kutambua dhambi na kuzikiri, kwa maana hiyo ndiyo mwanzo wa kumwendea Kristo. Mwanadamu akitambua dhambi zake na kukiri kwamba ni mwenye dhambi, amechukua hatua ya kwanza ya uponyaji. Yatambue maovu yako na ukiri dhambi zako sasa upate kuokoka na kuupata uzima wa milele kupitia kristo Yesu usijeukafa na msalaba wako wa dhambi na kuikosa mbingu.

Msalaba wa ukombozi:
Yeye Yesu Kristo Bwana wetu asiye na dhambi na aliyeishi maisha matakatifu duniani lakini kutokana na upendo mkuu aliokuwa nao juu yetu akaamua kufanyika dhambi kwa ajili yetu ili sisi tuweze kupona na kuwa huru. Na alisulubiwa kwa dhambi yote ya dunia hali yeye si mdhambi, (Isaya 53:4-5) aliteswa sana kwa mateso makali damu nyingi ilimwagika hadi akafa kutangua vifungo vyoye, mikataba yote, maneno yote, mzigo yote kwa maana hata biblia inasema “Damu ya Yesu inanena mema kuliko damu ya habeli”, Imenena mema kwangu inene kwako pia upate kuokoka na kupokea uzima wa milele. Huu msalaba wa matumaini ambao kupitia huo yesu alibeba dhambi za dunia hii ambazo hakuzitenda, alilipia deni la dhambi zetu, alilipia gharama kamili kwa damu yake na baada ya hapo akasema IMEKWISHA na kisha kuutoa uhai wake ili kumuharibu yule muovu, siku ya tatu alifufuka kutoka wafu na funguo za mauti na kuzimu. Tupo huru kabisa utukufu unayeye aliyethubutu na kuona ule ukuu na utukufu alikuwa nao ya kwamba si kitu akavaa mwili na kuamua kushuka dunia kwa hali ya umasikini ukilinganisha na utukufu aliokuwa na mbinguni ili kutuokoa sisi na kutufanya makuhani na wafalme wa dunia hii, libarikiwe na kuinuliwa jina lake YESU KRISTO milele na milele.

Fundisho hapo juu, tunaona mhalifu mmoja pembeni ya Yesu aliyekufa na dhambi zake na mhalifu mwingine mwenye dhambi aliepokea uzima pale msalabani na kufa pasipo dhambi. Na imeelezwa vizuri kabisa mhalifu yule aliyemkebehi alimuona Yesu kama mwanadamu wa kawaida na mhalifu mwingine alimuona kama Bwana, huyu wa kwanza alimuona kama mfalme wa kutaniwa na kudhihakiwa na wa pili alimwona kama Mfalme wa wafalme, huyu wa kwanza alimuona kama mwenye dhambi kama wao na wakati yule wa pili alimuona kawa mwokozi na akaokoka. Hawa watu wawili kila upande wa Yesu pale Golgotha wanawakilishi vile dunia inavyochukulia MAISHA YA YESU na mafundisho yako, kweli inagawanya. Yesu katika Mathayo 10:34 anasema mwenyewe msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani, la hasha bali upanga. Ushuhuda wa Yesu kristo siku hizi unazaa kibali upande mmoja na kukataliwa upande mwingine.

Maneno hayeleti mabadiliko lakini Imani yaleta, Kama huna imani na unaihitaji muombe Mungu sasa akupe kuwa na imani umwamini yeye na Neno lake katika Biblia takatifu. Na hutakuwa wa kwanza kupaza sauti “Bwana naamini; nisaidie kwa kutokuamini kwangu” Muite leo muombe akuokoe, akufutie dhambi zako na kukupa Uzima wa milele (Marko 9:24; Matendo16:31; Warumi 10:9-13; Yohana 1:12-13)