#SHINDA MAKWAZO YOTE KWA MEMA

Duniani kuna makwazo, shida na dhiki sana lakini kama biblia isemavyo jipe moyo kwa kuwa Yesu aliushinda ulimwengu na ni hakika yetu nasi kushinda tukiwa ndani yake Yesu, kwa maana makwazo yapo lakini imetupasa tuyashinde kwa mema na neno linatoa ole! kama onyo kwa yule ayasababishayo.
Yusufu nduguze walimkwaza sana yaani kila alipotaka kuzungumza jambo ambalo ni la Mungu kwa faida ya familia yake nduguze walimpinga na kumchukia sana, wakamtenga na kumfanyia mengi yakwazayo, yusufu alisonga mbele akimwamini Mungu ilifika wakati wakampiga vita kiasi cha kutaka kuutoa uhai wake kisa tu anayo neema na kibali cha Mungu lakini mwisho wa hayo yote ushindi ukawa dhahiri kwake.
Pia tunamsoma Ayubu vile alivyovunjwa moyo na kukwazwa sana na mke wake na rafiki zake kiasi ambacho yale majaribu yake isingekuwa neema kuu ya Mungu juu yake yamkini asingeweza kupita kutokana na makwazo hayo, mke aliongea yake na marafiki pia nao waliongea yao lakini yeye imani yake kwa Mungu ilikuwa kuu sana kiasi ambacho kwa kule kuwa na kila kitu halafu ghafula kukosa vyote hakukumfanya yeye amukufuru Mungu. Aliisimamia imani yake kwa Mungu katika shida na raha pamoja na makwazo yote hakuteteleka akajipa moyo mkuu na kujifariji mpaka akayashinda na wala hakuuchukua ushauri wa yeyote alikuwa yeye na imani yake kwa Mungu ndivyo vilivyompa moyo wa subira na kumfanya adumu katika ile imani na Mungu mwishowe akambariki maradufu.
Yesu Kristo ambapo Mungu alijifanyisha mfano wa mwanadamu na kuishi pamoja nasi kwa njia ya Yesu Kristo, aliishi maisha ya kawaida ya kibinadamu katika viwango vyote tuvipitiavyo na akaonyesha unyenyekevu na utii mkubwa sana kwa Mungu vile itupasavyo nasi kuishi mfano wake yaani yale maisha yake. Ndugu zake pale alipokuwa anatimiza kusudi lake la kuishi duniani walikuwa wakimkwaza pia na kutaka kutomuelewa kabisa ayapasayo kutenda duniani kiasi ambacho uhalisia wake wote hakuuonyesha nyumbani kwake bali ugenini na kwa watu wa kuja waliomwamini.
Yesu Kristo anajua katika makwazo, katika kuvunja mtu moyo ama kumupuuza kuna kufifisha na kuua kusudi la Mungu katika maisha ya viumbe vyake ndio maana aliasa katika Biblia kwamba waacheni watoto wadogo wamuendee yeye Yesu yaani wale waliomwamini na kuwa na kiu ya kutenda mapenzi ya Mungu na akasema mtu awakwazaye walio wadogo kama hao ni bora angefungiwa jiwe la kusagia na kutupwa baharini kuliko kuharibu na kudhoofisha kwa namna yeyote ile; dhamiri zao kuhusu Yesu kristo na utakatifu na imani yao kwake.
Ingawa kwa wanadamu ndio kawaida yao tena hasa wale wanadamu wa karibu yako watakuchunguza na kuangalia mwenendo wako na kisha kukujaribu wakiona kuna kitu wataanza kukuvunja moyo na kukupuuza, halafu wataanza kukucheka kwa maneno ya hapa na pale kisha wataanza kukupiga vita kila upande mwishowe unashinda.  Hivyo ndugu usikate tamaa wala kuvunjika moyo kwa maana katika kuvunjika moyo kuna kudumaa kiroho na kunajenga roho ya kujinyanyapa na pia kunaondoa ujasiri wako kiimani. Jua kuwa makwazo ukiyaruhusu ndani yako kunaongezeko la mawazo ambayo huondoa chocheo la imani rohoni na kukujengea moyo wa kughairi na kukata tamaa saa ingine.  Na makwazo hakika ni silaha ya shetani hata kama itatumiwa na mtu ambaye ni kiongozi wako au yule anayesimama mbele zako, kwa kuwa yanaweza kufifisha ama hata kuua majaliwa yako uliyopangiwa na Mungu kama tu utaruhusu makwazo yakutikise katika msimamo wa imani yako.
Yote katika yote yatupasa tumtazame Mungu mwenye enzi yote ndio kila kitu, kwa maana yule mkuu mbele yako aliyefanyika nafasi ya juu, umuchukuliaye kama bwana wako anaweza kuwa chanzo cha kukuinua ama kukuua kiroho na kisha kudumaza imani yako na mwisho kusudi la Mungu lililokuwa angavu mbele yako kufifia ama kutoweka kabisa lisiwe majaliwa yako.
Biblia inatufunza ya kwamba wale wajibidiishayo katika kuwaelekeza wengi katika njia ya haki yaani namna ya kuishi maisha matakatifu hao watang’aa kama nyota. Hivyo ni bora kuwa muhuishaji kuliko kuwa mfifishaji yaani kufufua na kuvifanya viishi vya rohoni vilivyokufa katika wengi pasipo fikra potofu kuliko kuvififisha na kisha kuviua kabisa vya rohoni vinavyotaka kuishi katika Bwana. Kwa hiyo basi kuna nguvu na dhawabu kubwa katika kuinua wengine kuliko kuwafifisha na kuwaua kiroho maana damu yao itatakwa mikononi mwao wafanyao hivyo.
Mungu baba katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti tupe moyo huo wa kuinua wengine na kushinda makwazo yote kwa mema kama biblia isemavyo tuushinde ubaya kwa wema, kuilinda imani yetu na kuwa wa upendo na baraka katika wewe, Ameni.

Rejea katika Biblia; Mwanzo sura ya 37-50 (kwa habari ya Yusufu), Kitabu cha Ayubu, Yohana 16:33, Marko 10:13-15, Luka 17:1-2, Danieli 12:3 na Rumi 12:21.

No comments:

Post a Comment