#USHINDI WA VITA VYA NDANI HUKUHAKIKISHIA USHINDI WA VITA VYA NJE

Huu nao ni ubatili mwingine, Mwanadamu huwaza na kupigana vita vya nje ya mwili wake zaidi kuliko hata apiganavyo na kutamani kuvishinda vita vitokotavyo ndani yako na ya kwamba amesahau kwamba vita kuu imusababishayo Mwanadamu kushindwa imo ndani ya maungo yake yaani ni ile ya kutokea ndani yake, na pale tu Mwanadamu awezavyo kushinda vita hivyo vya ndani ndivyo awezavyo kushinda vita vya nje na kuupinga ufalme wa giza hii ni uhakika kabisa.

Hebu waza hivi ni nini na ni wapi chanzo na asili ya vita vyote kama si ndani yetu wenyewe?  Biblia katika Yakobo 4:1 inasema, “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?”. Tunafikiria sana na kusema huu ni uchawi tu hakuna lingine, hii ni mizimu ya kwetu, haya ni mapepo machafu, ni majini tu yananifuatilia, ni watesi wangu wanao tamani nilichonacho, na kumbe Nguvu yao juu yetu ni ule udhaifu iliojidhihirisha ndani yetu na tulioshindwa kuushinda na wala si jingine.

Tunafikiri na kuwaza hivyo kwa sababu tumeshashindwa ndani yetu, hakuna kilicho na Nguvu juu yetu kama tu hatutakuwa na hatia na kinyume na Mungu. Yakobo 4:2-3 inasema, “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!, Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Hebu waza hivi kushindwa kwa Lucifa, shetani mbinguni kulikuwa ni kupigwa vita kutokea nje au ndani? kwa maana alishindwa kabisa na kibali cha Mungu juu yake kikafutwa kabisa na akatupiliwa mbali kabisa na kutengwa na Mungu na kuikosa ile nafasi na ahadi ya Mungu ndani yake, Ni kwambie ni ile vita iliyochipuka ndani yake kama jaribu na wala yeye hakuweza kuishinda na akashindwa na ndivyo kushindwa kwake vita vyote vya nje kulivyothibitika kwa maana hakuweza kuishinda ile dhambi ya kujiinua [pride] akawa msaliti wa Mungu.

Vimo vita ndani yetu ambavyo ni asili ya vita vyote vinavyotufuatilia na kama tu tungevishinda vita hivyo ufalme wa giza usingeona hatia ndani yetu na hivyo usingekuwa na hata nafasi ya kupigana nasi kwa maana ushindi wa ndani ndio uhakika wa ushindi wa vita vya nje. Tunapaswa kuiishinda tamaa iliyotukuka iwe ya uzinzi ama anasa zingine za dunia hii, tunapaswa kuiishinda ile hali ya kujiinua itusababishiayo dhambi ya kutokuwa wanyenyekevu, tunapaswa kushinda ubinafsi, wivu wa kuzidi, matusi, mawazo machafu ndani yetu, tunapaswa kuushinda uongo, masihara kwenye vitu na mambo ya msingi kabisa, nakuhakikishia pale tu tuyawezavyo na kuyashinda hayo hata shetani na ufalme wake huwa hana cha kutushitaki ama kutupiga vita kwa maana tunahesabika kuwa washindi kwa haki ya Mungu na neno (Yeremia 1:19; 15:20-21) watapigana nasi lakini hawatatushinda linathibitika hapo na wala sio sisi kupigana nao kwa maana vita vyetu kuu ni kuushinda mwili huu na asili ya mabaya yote yajichocheayo ndani yetu na kuzikomboa kabisa fikra zetu potofu tuwe huru. Kumbuka pia Yakobo 4:4 inasema, “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”

Namalizia hivi; sala zetu kwa msaada na uweza wa roho mtakatifu katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti ziwe ni, Mungu tuwezeshe kujishinda wenyewe yaani miili hii dhidi ya yote yaivutayo miili yetu kwayo ili tuwe na haki mbele zako Mungu Baba daima na shetani vita aielekezayo kwetu iwe ni ubatili na kushindwa kwake na sisi tuwe washindi daima, na kushinda kwetu vita vyote iwe ni kwamba tulishayashinda yote ndani yetu hivyo vita vya nje si kitu, Mungu tuwezeshe tuwe na imani hiyo na kukuamini wewe sana sana katika jina la Yesu Kristo, kwa ule ushindi wako pale msalabani ulituthibitishia ushindi wetu pale tu tutendavyo ya haki ya Mungu na kuzidi.

Siku zote kumbuka neno hili na ufahamu na kuelewa siri iliyopo ndani yake, isije kuwa na wewe ukawa ni mmoja wao wapigana nao vita vibaya. Soma mara kwa mara Yakobo 4:7-10 inayosema, “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.” Amina.

No comments:

Post a Comment